Monday, January 28, 2013

Je, watoto wetu wanajifunza? Utafiti wa uwezo wa watoto kusoma na kuhesabu Tanzania 2010


Matokeo Muhimu

Je, watoto wetu wanajifunza?
Utafiti wa uwezo wa watoto kusoma na kuhesabu
Tanzania 20101
Utangulizi
Kote nchini, maendeleo makubwa yamefikiwa kwenye elimu ya msingi ndani ya
muongo (miaka 10) uliopita. Uandikishaji umepanda maradufu kote elimu ya msingi
na sekondari, na mamilioni ya watoto wameweza kwenda shule. Tanzania iko mbele ya
muda wa kutekeleza na kuyafikia malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanayohusu
upatikanaji wa elimu na usawa wa kijinsia katika elimu. Madarasa maelfu yamejengwa na
maelfu ya walimu wameajiriwa. Bajeti ya elimu imeongezeka mara tatu zaidi kwa kipindi
hiki; Serikali sasa inatumia dola za kimarekani zaidi ya bilioni moja kila mwaka au karibu
Sh 1 kwa kila Sh 5 ya bajeti ya elimu.
Mafanikio haya siyo hatua rahisi; yalihitaji dhamira kubwa ya kisiasa na mgawo mkubwa
wa fedha za umma. Wazazi pia wamejitahidi kugharamia sehemu yao, maana hata
ile elimu ya bure kiuhalisia sio bure, maana kuna gharama za sare za shule, vitabu,
kalamu, masomo ya ziada, usafiri na mengineyo. Swali la msingi hapa ni – Je, jitihada
na uwekezaji huu mkubwa umezaa matunda gani? Je, watoto wetu wanauwezo
wa kusoma na kufanya mahesabu? Mantiki ya elimu ni kumsaidia kila mtoto kukuza
maarifa ili aweze kuishi maisha yenye ustawi ndani ya dunia – kwa kuanza kujua kusoma
na kufanya mahesabu stadi ambazo zinaweka msingi wa uwezo wa kudadisi, kufikiri,
kusikiliza, kuuliza maswali, kuchambua, kupambanua na kuwasiliana kwa kujiamini. Je,
shule zetu zinafanikiwa kwenye jukumu hili? Watoto wetu wanajifunza?
Juhudi ya Uwezo imeundwa kujibu swali hili muhimu, na ripoti hii inawasilisha matokeo
ya utafiti wake wa kwanza. Uwezo ni juhudi ya miaka minne inayofuatilia ubora wa
1 Muhutasari huu umeandaliwa na Uwezo Tanzania (www.uwezo.net).
Uwezo iko ndani TEN/MET (www.tenmet.org) na ni sehemu ya juhudi pana
ya Afrika Mashariki inayoratibiwa na Twaweza (www.twaweza.org)
2
ujifunzaji mashuleni kwa kupima uwezo wa watoto wenye umri kati ya miaka 5 na 16
kusoma na kufanya hesabu kwa wanafunzi. Juhudi hii nchini Tanzania iko ndani ya TEN/
MET (Mtandao wa Elimu Tanzania, www.tenmet.org); na ni sehemu ya juhudi pana ya
Afrika Mashariki ukizijumuisha pia nchi za Kenya na Uganda inayoratibiwa na Twaweza
(www.twaweza.org). Upimaji umezingatia mbinu bora iliyothibitika iliyoandaliwa na
Kituo cha ASER nchini India, na inatumia mbinu ya kisayansi kupata sampuli nasibu ya
kaya nchi nzima. Watafiti waliopatiwa mafunzo walizitembelea kaya na kupima stadi za
kusoma (Kiswahili na Kiingereza) na kufanya Hisabati kwa kila mtoto kwa kutumia jaribio
fupi la ngazi ya darasa la 2. Ngazi ya darasa la 2 imechaguliwa kwa sababu kwa mujibu
wa viwango vya kimataifa na Tanzania hadi kufikia mwisho wa mwaka wa pili wa elimu ya
msingi kila mtoto anapaswa kuwa tayari ana stadi za msingi za kujua kusoma na kufanya
hesabu.
Upimaji wa kwanza wa Uwezo nchini Tanzania ulifanyika Mei 2010, baada ya maandalizi
makubwa na upimaji wa majaribio. Ulihusisha wilaya 38 kati ya wilaya 133 za Tanzania.
Katika kila wilaya vijiji 30 vilichaguliwa kwa nasibu, na katika kila kijiji watoto wote wenye
umri kati ya miaka 5-16 katika kaya 20 walipimwa. Kwa ujumla, watoto 42,033 katika kaya
22,800 walipimwa uwezo wao katika stadi za msingi. Matokeo sita muhimu ya upimaji
huo yanawasilishwa hapa chini. Ripoti kuu inaweza kuchukuliwa hapa www.uwezo.net
Matokeo Muhimu
1. Mhitimu mmoja kati ya
wahitimu watano hawezi
kusoma Kiswahili cha ngazi ya
darasa la 2
Japo Kiswahili ni lugha inayozungumzwa
kwa upana zaidi nchini, idadi kubwa ya
watoto hawawezi kusoma Kiswahili bila
shida. Kwenye sampuli zetu, chini ya nusu
(42.2%) ya watoto waliofanyiwa uchunguzi
waliweza kusoma kwa hatua ya hadithi.
Wakati watoto wote katika darasa la
3 wanapaswa kuweza kusoma hadithi
ya ngazi ya darasa la 2, watoto chini ya
mmoja kati ya 3 (32.7%) ndio wanaweza.
Watoto wengi hawajifunzi kusoma hadithi rahisi hadi wafikie darasa la 5 au la 6.
Hata hivyo, hadi wanamaliza shule ya msingi, mtoto mmoja kati ya 5 hawezi kusoma
hadithi ya ngazi ya darasa la 2. Licha ya kumaliza miaka saba ya elimu ya msingi,
watoto hao wanaelekea kubaki mbumbumbu (hawajui kusoma na kuandika) maishani
mwao.
3
ASILIMIA YA WATOTO WANAOWEZA KUSOMA KISWAHILI NGAZI YA DARASA LA 2
Darasa Hajui kitu Herufi Neno Aya Hadithi Jumla
Awali 53.5 27.7 2.7 2.5 13.6 100
Darasa la 1 41.8 37.8 10.6 4.2 5.6 100
Darasa la 2 24.1 32.3 17.0 9.8 16.8 100
Darasa la 3 14.8 20.0 16.4 16.1 32.7 100
Darasa la 4 9.6 14.7 12.0 16.6 47.1 100
Darasa la 5 6.0 10.1 7.4 13.8 62.8 100
Darasa la 6 4.0 6.1 4.9 11.1 73.9 100
Darasa la 7 1.8 5.9 3.3 8.0 81.0 100
Jumla 18.6 19.2 9.6 10.5 42.2 100
2. Nusu ya wanafunzi hawawezi kusoma Kiingereza cha ngazi ya
darasa la 2
Kiingereza ni somo gumu zaidi
kwa wanafunzi. Ingawa wanafunzi
wote wa darasa la 3 wanapaswa
kuweza kusoma Kiingereza cha
ngazi ya darasa la pili, chini ya
mwanafunzi 1 kati ya 10 (7.7%)
ndio anaweza. Maendeleo kwenye
somo la Kiingereza ni ya taratibu
sana; kwa darasa la tano, ni mtoto
1 tu kati ya watoto 4 anaweza
kusoma hadithi. Karibu nusu ya
wanafunzi hawawezi kusoma hata
maneno mafupi ya Kiingereza.
Watoto wengi wanafika darasa
la 7 bila kuwa na stadi zozote za
Kiingereza. Hadi wanamaliza shule
ya msingi, nusu ya wanafunzi (49.1%) bado hawawezi kusoma hadithi ya kiwango
cha darasa la 2 ya Kiingereza, na bila shaka wanafunzi wachache sana wanauwezo wa
kusoma kwenye ngazi ya darasa la 7. Hii ina maana kuwa idadi kubwa ya wanafunzi
wanaoingia sekondari hawawezi kusoma kwa lugha ya Kiingereza, ambayo ni lugha
ya kufundishia elimu ya sekondari.
4
ASILIMIA YA WATOTO WANAOWEZA KUSOMA KIINGEREZA NGAZI YA DARASA LA 2
Darasa Hajui kitu Herufi Neno Aya Hadithi Jumla
Awali 68.3 16.9 2.3 3.4 9.1 100
Darasa la 1 68.0 24.8 3.8 1.3 2.1 100
Darasa la 2 55.5 29.4 7.5 3.8 3.9 100
Darasa la 3 42.0 26.7 14.2 9.4 7.7 100
Darasa la 4 29.0 24.0 16.0 15.5 15.4 100
Darasa la 5 21.4 19.6 13.7 20.9 24.5 100
Darasa la 6 15.1 13.6 13.6 21.9 35.8 100
Darasa la 7 7.9 11.5 10.7 19.1 50.9 100
Jumla 37.8 21.0 10.4 12.1 18.7 100
3. Wahitimu 7 tu kati ya 10 wanaweza kufanya hesabu za ngazi ya
darasa la 2
Ingawa stadi za kuzidisha ziko kwenye
mtaala wa darasa la 2, wanafunzi
wachache tu wa darasa la 2 waliweza
kuzidisha bila shida. Zaidi ya
nusu ya wanafunzi hawawezi hata
kujumlisha. Hadi kipindi wanafika
darasa la 5, watoto wengi wanaweza
kutoa na kujumlisha, lakini wengi
bado hawawezi kuzidisha. Watoto
wengi wanapata stadi za Hisabati
mwishoni mwa shule ya msingi.
Hata hivyo, watoto 3 kati 10 (31.5%)
wa darasa la 7 bado hawawezi kufanya
hesabu za kuzidisha za ngazi
ya darasa la 2. Na mtoto 1 kati ya 10 anamaliza shule ya msingi bila kuwa na stadi
za Hisabati kabisa; hawezi hata kujumlisha hesabu ndogo. Hii inaweza kumaanisha
kuwa watoto wengi wanaojiunga na shule za sekondari hawana msingi imara kwenye
Hisabati ambao ni muhimu kwenye ujifunzaji na uchambuzi, hasa katika masomo ya
sayansi na biashara.
5
Kijijini
Mjini
Awali
Darasa I
Darasa II
Darasa III
Darasa IV
Darasa V
Darasa VI
Darasa VII
ASILIMIA YA WATOTO WANAOWEZA KUFANYA HISABATI NGAZI YA DARASA LA 2
Darasa Hajui kitu Namba Kujumlisha1 Kujumlisha2 Kutoa1 Kutoa2 Kuzidisha Jumla
Awali 40.0 41.9 2.7 1.6 1.7 1 11.0 100
Darasa la 1 26.5 56.9 9.2 1.9 2.3 1 2.4 100
Darasa la 2 15.7 45.8 16.9 4.9 5.5 4 7.6 100
Darasa la 3 9.9 30.3 20.0 8.5 7.3 6 18.5 100
Darasa la 4 7.2 22.0 14.1 10.0 7.0 7 32.8 100
Darasa la 5 5.1 13.9 11.0 10.3 6.7 7 45.8 100
Darasa la 6 3.3 9.2 7.7 10.2 5.9 6 57.8 100
Darasa la 7 2.2 7.9 4.8 7.0 4.7 5 68.5 100
Jumla 13.1 28.3 11.1 7.0 5.2 5 30.8 100
4. Watoto wa mijini hufanya vizuri zaidi kuliko wa vijijini
Watoto wa mijini hupata asilimia kati ya 7 na 10 zaidi kuliko watoto wa vijijini katika
masomo yote. Tofauti ni kubwa zaidi hususani katika madarasa ya 2-4, wakati watoto
wa mijini huanza kupata stadi za msingi ilhali wenzao wa vijijini wanaachwa nyuma.
Inaelekea kuwa watoto wa vijijini hatimaye huanza kupata stadi hizo za darasa la pili
wafikapo madarasa ya 6 na 7; lakini kuna uwezo mkubwa kuwa wanazidi kuporomoka
zaidi kwenye stadi ya kusoma katika ngazi yao
5. Wasichana hufanya vizuri kuliko wavulana
Wasichana walifanya vizuri zaidi katika masomo yote waliyopimwa, ingawa tofauti
ni ndogo sana. Kati ya watoto wote waliopimwa, 43.5% ya wasichana waliweza
kusoma hadithi katika Kiswahili ikilinganishwa na 40.7% ya wavulana. Katika masomo
ya Kiingereza na Hisabati tofauti ilikuwa ni ndogo mno, kama inavyooneshwa katika
jedwali hapo chini. Hata hivyo matokeo haya yanapingana na ile dhana ya muda mrefu
6
% Watoto
Hadithi ya Kiswahili Hadithi ya Kiingereza Kuzidisha
Wavulana
Wasichana
Hawako shule Awali Elimu ya watu wazima Msingi 1-4 Msingi 5-7 Sekondari +
% Watoto wanoweza kusoma
kuwa wasichana hawafanyi vizuri kama wavulana, na inaibua maswali kuhusu kwa nini
kunakuwa na tofauti kubwa katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi
ambapo wavulana hung’ara zaidi. Hata hivyo, tofauti hizi ndogo zisifiche ule ukweli
mkubwa zaidi kuwa watoto wengi mno wasichana na wavulana hawana uwezo wa
kimsingi katika masomo ya lugha zote mbili na Hisabati.
6. Watoto wenye mama waliosoma hufanya vizuri zaidi
Watoto ambao mama zao wamesoma hadi elimu ya sekondari hufanya vizuri sana
kuliko watoto wengine. Kwa mfano, katika darasa la 3 na 4 watoto hawa wana
uwezekano wa mara tano zaidi kuweza kusoma hadithi ya Kiingereza na wana
uwezekano wa mara mbili zaidi kufanya Hisabati na kusoma hadithi ya Kiswahili. Hata
watoto ambao mama zao wamemaliza elimu ya msingi tu wanafanya vizuri kiasi kuliko
wale ambao mama zao hawajasoma kabisa. Tofauti katika matokeo huanza kujionesha
kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba; ikiashiria kwamba elimu ya mama ni
muhimu katika ngazi zote za shule.
7
Hitimisho
Matokeo ya tathmini ya Uwezo iliyohusisha kaya zaidi ya 20,000 na watoto zaidi
ya 40,000 yanaonesha kuwa kuna tatizo kubwa katika elimu nchini Tanzania. Hadi
wanapoingia darasa la 3, watoto asilimia 100% wanapaswa kuwa na stadi za kusoma
na kuhesabu. Lakini ukweli ni kuwa hadi darasa la 3, watoto 7 kati ya 10 hawawezi
kusoma Kiswahili cha msingi; watoto 9 kati ya 10 hawawezi kusoma Kiingereza cha
msingi, na watoto 8 kati ya 10 hawawezi kufanya Hisabati za msingi.
Hata wanapofikia hatua ya kumaliza elimu ya msingi idadi kubwa mno ya watoto huwa
hawawezi kufanya kile ambacho walipaswa kuwa wana kijua miaka mitano iliyotangulia
wakati wakiwa katika darasa la 2. Mgawanyo kiwilaya unaonesha tofauti kubwa kati yao,
na ambapo baadhi ya wilaya ziko chini sana ya wastani wa kitaifa.
Ukweli ulio bayana ni kuwa, licha ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika elimu
yaliyowezekana kutokana na kuwekezwa kwa matrillioni ya shilingi kila mwaka, idadi
kubwa sana ya watoto nchini Tanzania hawajifunzi.
Je, nini kifanyike kuhusu hali hii?
Kwanza, tunahitaji kutulia na kutafakari matokeo haya na kuchunguza yanamaanisha nini.
Kukimbilia kuyapuuza au kutunga masuluhisho ya haraka haraka pengine haitasaidia,
kwani inaweza kusababisha kushindwa kutambua kiini cha tatizo na hivyo kuchukua
hatua zisizofaa. Kushangilia majengo mapya na idadi kubwa ya watoto wanaoandikishwa
shule inaweza kuwa hatari kama matokeo yake ni kufunika ukweli kwamba idadi kubwa
ya watoto wanamaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma na kuhesabu.
Pili, ingawa changamoto lazima ziwepo pale ambapo mfumo wa elimu unapopanuliwa
ghafla, bado tunaweza kuuliza: Je, mikakati ya kisera na malengo ya kisiasa yanalenga
mambo sahihi? Hivi sasa, nchini Tanzania na kwingineko, mkazo zaidi umewekwa
katika kupatikana kwa vitendeakazi kama vile madarasa, maabara, vitabu na walimu,
badala ya matokeo ya ujifunzaji. Mathalani, stadi za kusoma, kuhesabu, kuandika
udadisi na ubunifu. Kwa vile ushahidi unaonesha kuwa vitendeakazi havijaleta stadi hizi,
kuna umuhimu wa kupanga mfumo mzima wa elimu kulenga zaidi uwezo na stadi za
mwanafunzi, kuanzia ndani ya wizara zinazohusika na elimu, taasisi za elimu, watunga
mitaala, mitihani, tathmini ya walimu na shule, vipimo vya maendeleo na vipaumbele
vya kisiasa.
Tatu, kuna haja ya kuangalia zaidi nini kinachotokea shuleni kuliko kutazama takwimu
za kitaifa pekee. Tafiti zilizofanyika katika nchi nyingi zinaonesha kuwa mchakato wa
kufundisha na kujifunza unaweza kuwa na hitilafu kubwa. Mawili kati ya matatizo
ambayo hujitokeza mara kwa mara ni kuwa shule hazipati fedha za kutosha (yaani bajeti
za elimu zinazoongezeka zinatumika kwa mambo mengine badala ya kuboresha shule) na
kwamba walimu hawana motisha ya kutosha na hawafundishi (yaani muda wanaotumia
kufundisha darasani ni mdogo mno). Pengine itasaidia kuchambua mambo hayo mawili
8
kwa kina, na kutafuta namna ya kuyaboresha. Pia kuna haja ya kuangalia kwa makini
uhusiano kati ya rasilimali za kutosha kufika shuleni na walimu kuwapo kazini kwa
upande mmoja, na uwezo na stadi za mwanafunzi anapohitimu kwa upande mwingine.
Nne, uwazi zaidi unaweza kuwawezesha watunga sera na watu wengine kutafakari
na kuchukua hatua. Uwezo imedhamiria kusambaza matokeo ya tafiti zake ili kusaidia
kulifikia lengo hili. Lakini Serikali inaweza kwenda mbele zaidi ili kuwezesha data za kila
shule kupatikana kwenye mtandao, na katika vyombo vya habari kila afisa wa serikali
ya mtaa, mwalimu, mzazi na mwanafunzi alinganishe hali na utendaji wake na wa
wengine. Maendeleo ya teknolojia hasa usambazaji wa simu za mkononi vimewezesha
ubadilishanaji habari katika kiwango kikubwa na kufungua fursa mpya nyingi.
Tano, badala ya kuendelea kufanya kile ambacho kimeshafanyika kwa jitihada zaidi,
pengine umefika wakati wa kufanya kitu tofauti. Utafiti wa Uwezo na tafiti zilizofanyika
duniani zinaashiria kuwa kiini cha kitendawili hiki ni kuangalia upya suala la motisha ili
wadau muhimu katika sekta hii watambuliwe kwa kuhamasisha kujifunza. Wazo moja
ambalo linafaa kufikiriwa, na ambalo Rais Jakaya Kikwete kesha lipokea, linaitwa cash on
delivery au malipo baada ya matokeo (www.cgdev.org/section/initiatives/active/codaid).
Msingi wake mkuu ni kuwa kupatikana kwa fedha zaidi kwa kazi ya elimu kutategemea
kufikiwa kwa malengo (yaliyokaguliwa na shirika huru), kama vile kusoma na kuhesabu
(kwa mfano kwa kila mtoto anayemaliza elimu ya msingi akiwa na stadi zilizokubalika,
zitatolewa Sh laki tatu). Wazo hili linaweza kupanuliwa ili hizo Sh laki tatu zigawiwe kwa
viongozi wa eneo ilipo shule, walimu, na pengine hata wazazi. Lengo ni kuwashawishi
wadau wahusika kuzingatia na kutambua mafanikio katika kujifunza. Hakuna hakikisho
kuwa wazo hili litafanikiwa. Lakini katika hali ya kuwepo kwa tatizo kubwa linaloikabili
sekta ya elimu Tanzania kwa sasa, hasa pale ambapo njia za kawaida zimeshindwa kuleta
mafanikio ya maana, kufanya majaribio mbadala yaliyofikiriwa kwa makini kama hii
ya malipo baada ya matokeo, na kisha kuchunguza matokeo yake inaweza kutusaidia
kusonga mbele.
Matokeo ya utafiti wa Uwezo yanazinduliwa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu
nchini Tanzania. Vyovyote matokeo ya siasa yatakavyokuwa, miaka mitano ijayo inatoa
fursa ya kulitazama sakata la elimu kwa uwazi, ujasiri na kwa njia itakayoleta mafanikio.
Ni watu wenye stadi, uwezo na wanaojiamini watakao liwezesha taifa letu kuneemeka
hususani katika muktadha wa ushirikiano wa Afrika Mashariki na katika hali ya
utandawazi. Yeyote atayechaguliwa kuwa Rais ajaye wa Tanzania, kazi ya kuibadili elimu
kutoka kuangalia vitendeakazi hadi kuhakikisha kila mtoto anaweza kusoma na kuhesabu
na kujifunza pengine ndicho kitakuwa kipimo kikuu cha mafanikio ya uongozi wake.

Ripoti ya Utafiti wa TAMWA 2012 kuhusu Ukatili wa Kijinsia katika Jamii Tanzania Bara


 

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2012/07/Baadhi-ya-waandishi-wa-habari-kutoka-vyombo-mbalimbali-wakisikiliza-taarifa-ya-utafiti-huo1.jpg
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakisikiliza taarifa ya utafiti huo
RIPOTI YA UTAFITI WA TAMWA KUHUSU UNYANYASAJI WA KIJINSIA
1.0 UTANGULIZI
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), katika mpango mkakati wake wa miaka mitano 2000-2014, pamoja na mambo mengine kimepanga kufanya shughuli ambazo zitaimarisha elimu kwa mtoto wa kike kwa kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa vile vinavyoathiri wanawake na watoto. Vitendo hivyo ni pamoja na ubakaji, kulazimisha watoto wa kike kukatisha masomo na kuolewa, ukeketaji na familia kutelekeza watoto ambavyo kwa pamoja vinamnyima mtoto wa kike haki yake ya msingi ya kupata elimu. Kwa sababu hiyo, baada ya utafiti uliofanyika Februari 2012 katika shule za sekondari za kata kwenye mikoa 20 nchini kuchunguza mambo yanayochangia wanafunzi kukatisha masomo hasa kwa ujauzito na wengi kufeli mitihani ya taifa, mwezi Aprili 2012 TAMWA imefanya utafiti mwingine wa kihabari (journalistic survey) mwingine katika mikoa 20 ikiwepo 15 ya Tanzania Bara na Mitano ya Zanzibar kuhusu hali ya vitendo vya ukatili nchini. Vitendo vilivyolengwa ni ubakaji, vipigo kwa wanawake, kutelekeza wanawake na watoto, ukeketaji na kulazimisha watoto wa kike kulazimishwa kukatisha masomo na kuolewa.
TAMWA imepata msukumo wa kufanya utafiti huu wa kihabari kutokana na ukweli kwamba matendo haya ya kikatili yameshamiri s nchini, na hakuna utafiti wa hivi karibuni ambao ungesaidia vyombo husika kupima kiwango halisi cha matendo na matukio haya. Taarifa zilizokuwapo hadi utafiti huu unafanyika, kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa wa mwaka 2010, ni kwamba zaidi ya asilimia 39 ya wanawake nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili tangu wakiwa na umri wa miaka 15. Watuhumiwa wa unyanyasaji huu kwa kiwango kikubwa ni wanaume. Ripoti ya Polisi Zanzibar inasema katika mwaka 2011, yalikuwapo matukio 268 ya unyanyasaji yaliyoripotiwa; lakini kesi zilizofikishwa mahakamani ni 55 tu. Katika zote hizo, kesi moja ndiyo iliyomtia mtuhumiwa hatiani.
Kutokana na hali hii, na kwa kuzingatia mkinzano wa kisheria kati ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 juu ya umri wa mtoto kuolewa, na adhabu anayostahili, TAMWA imefanya utafiti kuona jinsi ya kupunguza ukatili wa wanawake kupitia habari za ushahidi wa matendo hayo na kupendekeza suluhisho muafaka. Lengo kuu la utafiti huu limekuwa ni kukusanya taarifa za awali zinazoonyesha halisi ya ubakaji, watoto wa kike wanafunzi kulazimishwa kuolewa, ukeketaji, vipigo kwa wanawake na watoto na wanawake kutelekezwa ili kujenga msingi wa kisayansi juu ya chanzo cha ukatili huo na kutafutua ufumbuzi.
2.0 WILAYA ZA UTAFITI
Utafiti huu ulifanyika katika wilaya moja kila mkoa wenye mikoa 20 ambayo ni: Morogoro (Mvomero), Mtwara (Newala), Shinyanga (Kahama), Dar es Salaam (Ilala, Temeke na Kinondoni), Kilimanjaro, (Same), Pwani (Mkuranga) Mara (Tarime), Manyara (Simanjiro),Tanga (Handeni), Kigoma (Kasulu), Iringa (Kilolo), Mbeya (Rungwe) Singida (Iramba), Dodoma (Kondoa ), Arusha (Karatu) na Njombe (Njombe). Mikoa ya Zanzibar na wilaya zake kwenye mabano ni Kaskazini Pemba, (Micheweni na Wete), Kusini Pemba (chakechake) Kaskazini Unguja (Kaskazini A, Kaskazini B), Kusini Unguja (Kusini Unguja), Mjini Magharibi (Wilaya ya kati). Hata hivyo ripoti hii inatokana na taarifa za wilaya 15 za Tanzania Bara. Ripoti ya Tanzania Visiwani imeandaliwa na ofisi ya TAMWA na TAMWA Zanzibar itazinduliwa huko Zanzibar.
3.0 WATAFITI NA MBINU ZA UTAFITI
TAMWA iliandaa dodoso ambalo liliwaongoza wanahabari watafiti katika kukusanya taarifa; kikaandaliwa kikao kifupi cha kuwaandaa wanahabari hao, na kila mshiriki akapewa nakala ya dodoso. Baadaye wanahabari walipewa barua za utambulisho ili kuwarahisishia utambulisho katika maeneo ya kazi, na kila mtafiti alishauriwa kuchagua kata tatu katika wilaya alikotumwa, na akashauriwa afanya utafiti wake katika vijiji vitatu – kimoja kutoka kila kata. Kwa kuwa ulikuwa utafiti wa kihabari, wahusika walishauriwa kutumia mbinu za kihabari kupata taarifa zao. Vyombo vya habari ambavyo TAMWA ilivishirikisha katika kufanya utafiti huu ni Tanzania Daima, Mwananchi, Jamhuri, The Guardian, ITV, The Citizen, Daily News, Nipashe, Majira, Habari Leo, The African, Mtanzania, Uhuru, The Habari.com, Dira, na TAMWA.
4.0 MAENEO YALIYOTAFITIWA
Utafiti huu uliweka kipaumbele katika maeneo matano ambayo ni: ubakaji, wanafunzi kulazimishwa kuolewa, wanawake kupigwa, wanawake na watoto kutelekezwa, na ukeketaji. Kwa kila eneo, utafiti ulilenga kuibua chanzo, ukubwa, athari, na pendekezo la ufumbuzi wa tatizo.
5.0 CHANGAMOTO ZA UTAFITI
Miongoni mwa changamoto zilizowakabili watafiti ni woga wa wahusika katika kuzungumzia unyanyasaji. Baadhi yao walidhani kwamba taarifa zinazowahusu zikitolewa kwenye vyombo vya habari zingeweza kusababisha wao kudhurika au kushitakiwa. Katika baadhi ya maeneo, miundo mbinu ilikuwa mibovu na kusababisha watafiti kuchelewa kufika na kuanza kazi mapema. Urasimu wa baadhi ya viongozi ulichangia kukwamisha upatikanaji wa takwimu katika maeneo kadhaa. Baadhi ya wahojiwa walitaka walipwe kabla hawajatoa taarifa walizonazo.
6.0 MATOKEO YA UTAFITI
Kijumla, matokeo kutoka mikoa mbalimbali yameonyesha kwamba ukatili wa kijinsia ni moja ya matatizo ya msingi katika jamii yetu. Sababu na mazingira ya ukatili huo yanashahabiana kwa sehemu kubwa; na baadhi ya mapendekezo yanafanana. Kilicho dhahiri ni kwamba mkinzano wa kisheria kuhusu umri wa mtoto kuolewa, na mila na desturi za baadhi ya makabila katika mikoa husika, ni mambo yanayochangia kushamiri kwa matukio ya unyanyasaji huu wa kijinsia.
6.1 UBAKAJI
Dhana ya ubakaji ni pana kijamii na kisheria. Kijamii, ubakaji katika maeneo mengi umeelezwa kama ngono ya kulazimisha; lakini kisheria, ni pamoja na kufanya ngono na mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18, hata kama amekubali. Kwa sababu hiyo, taarifa juu ya ubakaji zipo nyingi vijijini, hasa katika maeneo ambayo watoto huolewa wakiwa chini ya miaka 18. Katika baadhi ya mikoa, yamedhihirika matukio ya ubakaji ambayo husababishwa na mabavu ya baadhi ya wanaume, ulevi, matumizi mabaya ya kipato, malezi duni, ushirikina, umaskini wa wasichana na wazazi wao, na tamaa mbaya ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye aibu wasioweza kujadiliana na wanawake kuhusu taama yao hiyo. Kimsingi, ubakaji ni tatizo la kitaifa; na moja ya njia za kulipunguza ni kubadili sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ili kuzuia wanaume kuoa watoto wa kike walio chini ya miaka 18. Lakini kingine kikubwa kilichojitokeza na ambacho kinahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka ni kwamba wahusika wengi wa ubakaji hawafikishwi mahakamani na wale wanaofikishwa mahakamani wanaachiwa huru kutokana na vyombo vya kutoa haki kugubikwa na rushwa na kukosekana kwa ushahidi kutokana na wananchi kutokujua jinsia ya kutunza ushahidi wa ubakaji. Ili ushahidi wa ubakaji uwe dhahiri, mtu aliyebakwa anapaswa asioge wala kubadilisha nguo alizokuwa amevaa wakati anabakwa na anatakiwa kuwahishwa polisi kupata PF3 na kisha kwenda hospitali kupimwa kupata ushahidi na kupatiwa dawa tiba na kuzuia maambukizi ya magonjwa hatari kama vile virusi vya UKIMWI. Lakini pia kuna unyanyapaa mkubwa kwenye jamii kuhusu suala zima la ubakaji. Jamii bado inauonea haya uovu huu ambao unachangia kwa kiasi kikubwa mimba mashuleni na maambukizi ya virusi vya UKIMWA.
6.1.1 Visa Mkasa:
(a) Katika Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, yapo matukio ya wanaume kufanya ngono na watoto wadogo, lakini hatua kali hazichukuliwi. Upo mfano wa mtoto mdogo wa miaka 10 aliyetoroshwa na kijana, akaacha shule. Ofisa Mtendaji alipoletewa taarifa hizo alimchukua mtoto huyo na kumpeleka hospitali, hatimaye polisi wakaanza kumsaka mtuhumiwa. Lakini mtoto amekataa katakata kurudi shuleni. Tatizo kubwa ni kwamba wazazi wengi hawako tayari kufikisha masuala haya polisi, na hata wanaposaidiwa kufanya hivyo, wasichana na wazazi hawapatii polisi ushirikiano. Watuhumiwa wengi huachiwa huru.
(b) Hali ni ile ile katika Wilaya ya Njombe, Mkoa wa Njombe, ambako usiri wa jamii kuhusu matukio haya umefanya mengi yapite bila kuripotiwa; huku baadhi ya watendaji wakikana kabisa kuwapo kwa matukio hayo. Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya, Sarah Dumba anasema: “Matukio haya hufanyika hata kwa mzazi kumbaka mtoto au mtoto kumbaka mzazi na kwamba matukio haya huripotiwa Polisi na pia hunifikia kwa sababu tunafanya kazi na Polisi kwa ukaribu na ushirikiano ambapo matukio ya ubakaji 37 kuanzia Julai mwaka 2011 hadi Aprili mwaka huu (2012) yalinifikia, pamoja na imani za kishirikina pia wapo wanaobakwa kwa sababu tofauti, hawa wamekuwa wagumu kuripoti polisi na kuja kutoa ushahidi pindi kesi inapofikishwa mahakamani, hivyo mahakama inakosa ushahidi wa dhati wa kumtia mtu hatiani.”
Taarifa za Mahakama ya Wilaya ya Njombe zinaonyesha kuwa kesi 28 za ubakaji zimewahi utolewa uamuzi, na nyingine 28 zinaendelea.
(c) Kuhusu ubakaji usababishwao na ulevi, Alphonce Chaula, Mkazi wa Kijiji cha Mtwango, Kata ya Mtwango, anasema: “Utakuta mwanamke amekaa kilabuni ananunuliwa pombe anakunywa bila kuuliza pombe hiyo ananunuliwa kwa maana gani; akitoka hapo kuelekea kwake mwanaume aliyemnunulia pombe anamvizia na kumbaka. Kesho yake wanasema sababu ni pombe tu yanaishia hivyo. Wanawake wengi hasa ambao hawajaolewa wanabakwa sana, lakini wanaona aibu kuripoti kwani wanahisi kama watajidhalilisha na watakosa waume wa kuwaoa. Cha muhimu hapa ni kuwa wazi tu, kwani mficha maradhi mwisho wa siku kifo humuumbua,”
(d) Mkoani Pwani, Katibu wa Dawati la Jinsia, Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Mkuranga, Pascal Machangu, anasema kwa mwaka 2011 pekee walipokea kesi 18. Miongoni mwa hizo, kesi za ubakaji halisi ni 10; na zinazohusu kuwapa mimba wanafunzi ni kesi nane (8). Kesi tano tayari zimeshatolewa uamuzi; tatu bado zipo mahakamani.
(e) Wilayani Temeke, Dar es Salaam, kuna mtoto aliyebakwa akiwa na umri wa miaka tisa (9) tu. Mzazi wake, Mohammed Nassoro, anasema; “Mtoto wangu Latifa alibakwa mwaka jana akiwa na umri wa miaka 9, kesi ipo mahakamani na mtuhumiwa yupo nje. Kwa kweli kitendo cha mtoto kubakwa kinachangia maambukizi ya Ukimwi. Kwa upande wa mwanangu nashukuru yuko salama.”
(f) Wilayani Kahama, Shinyanga, lipo tukio la mwaka 2011 la mwanaume mfanyabiashara mwenye miaka 40 aliyemnajisi mtoto wa miaka mitano (5).
(g) Katika Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni, madaktari wanasema wanapokea matukio ya ubakaji yasiyopungua matatu (3) kila siku. Waliohojiwa wamesema chanzo ni ulevi wa pombe, uvutaji wa madawa ya kulevya na ahadi zisizotimia kutoka kwa wasichana. Elias Aman Akamwile (57), Mjumbe wa Mtaa Bunju B, Kata Mabwepande, anasema: “Wasichana wanabakwa kwa sababu wanapeana ahadi za mapenzi halafu baadaye wanakataa kutimiza ahadi hiyo, ndipo mwanaume anamvizia ili akufanyie kwa nguvu. Wanaobaka lazima huwa wanalipiza visasi, hawabaki bila sababu.”
Katika kituo cha Polisi cha Wazo Hill, mwaka 2010 ziliripotiwa kesi za ubakaji 71; na miongoni mwa hizo, 24 zilifikishwa mahakamani. Kesi nne (4) ziliamuliwa, 47 zikafutwa. Mwaka 2011 kesi za ubakaji 88 ziliripotiwa polisi; miongoni mwa hizo 32 zilifikishwa mahakamani. Kesi 56 bado ziko katika upelelezi. Mwaka huu 2012, kati ya Januari na Machi, kesi za ubakaji ziizoripotiwa ni 37. Zilizofikishwa mahakamani ni kesi 10; na kesi 27 ziko katika upelelezi.
6.2 WANAFUNZI KULAZIMISHWA KUOLEWA
Wanafunzi kulazimishwa kuolewa nalo ni tatizo la kitaifa ambalo limejitokeza katika mikoa yote. Wengi wao huolewa wakiwa na umri wa miaka 12 hadi 16. Sababu kubwa zinazotajwa ni umaskini wa wazazi, watoto kushindwa shule, ujauzito, tamaa za wanafunzi wenyewe, na migogoro ya kifamilia.
6.2.1 Visa Mikasa
(a) Veice Ngwada (32), Muuguzi katika Hospitali ya Mbweni, kitengo cha kuzalisha, Kata Mbweni, Kinondoni, Dar es Salaam, anasema baadhi ya watoto wanaozalia pale wana umri wa miaka 14 hadi 18. Mwaka 2010 walikuwa 18 watoto wajawazito 52 wenye umri wa miaka 15-18. Mwaka 2011 watoto wajawazito 20 walikuwa na umri wa miaka 14 hadi 17; waliokuwa na miaka 18 walikuwa watoto 22.
(b) Sharifa Rashid (14), Kidato cha Kwanza, Shule ya Sekondari Mabwe, anasema: “Nilisoma na rafiki yangu la kwanza hadi la nne akaja akafeli. Aliacha shule akiwa darasa la nne; alishindwa mtihani kwa kuwa alikuwa mtoro, ataniambia anataka kuolewa. Nafikiri kwa sababu aliishia darasa la nne anaona akiolewa atapata faida kwa mumewe. Wazazi wanaona anaweza akapata mimba ambayo haina baba, hivyo wanaona ni bora wamuozeshe ili azae kwa mume kuliko kubebea mimba nyumbani.”
(c) Katika baadhi ya shule mkoani Pwani, walimu wamekuwa wakigombana na wazazi ambao hawataki watoto wao wafaulu kwenda sekondari, kwa kuhofia kwamba akiendelea na masomo atachelewa kuolewa. Ofisa Elimu wa Wilaya ya Mkuranga anasema mwaka 2011 kulikuwa wanafunzi 15 wa sekondari waliripotiwa kuwa na mimba, na hivyo kukatisha masomo; watatu walifikishwa polisi, watatu mahakamani; na mmoja kwa mtendaji kata. Wazazi wa watoto wanane (8) hawakuchukua hatua yoyote.
(d) Mkurugenzi wa Mtendaji wa Wilaya ya Kahama Eliza Bwana anasema ndoa za kulazimisha watoto ni nyingi katika eneo lake kutokana na mila na desturi za wakazi wa eneo hilo. Baadhi yao huwatoa watoto shuleni na kuwaoza kwa wanaume wasio chaguo lao, kwa vile wanakuwa wameshapokea mahari kisirisiri. Kwa sababu hiyo, wazazi kama hao hulazimisha watoto wao wafeli mtihani wa darasa la saba ili waolewe. Anasema mtoto wa shule ambaye wazazi wake wameshapokea mahari hufikia mahali wazazi wake wanamuita “mtoto wa watu” kwa maana kwamba ni mke wa mtu! Kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa Wilaya, Jacqueline Ntulo, wasichana katika jamii hiyo hutazamwa kama mtaji; na masahibu haya huwapata watoto wenye umri mdogo kuanzia miaka 12 na 13.
(e) Ndoa nyingine za umri mdogo huchangiwa na mazingira magumu ya shule, ukiwamo umbali kutoka nyumbani hadi shuleni. Wilayani Mvomero, Morogoro, Mtendaji wa Kata ya Kanga, Buhatwe Matage, anasema wasichana hupata mimba na kuolewa kutokana na wazazi kushindwa gharama za kulipia elmu yao, lakini pia wapo wanaoathiriwa na umbali.
Anasema: “Umbali wa shule unaosababisha watoto kuamua kuolewa kuepuka mateso ya mwendo wa kasi na kushinda na njaa kwa siku nzima kutokana na kukosekana kwa chakula shuleni hivyo jamii inatakiwa kupewa elimu ya umuhimu wa kupata elimu kwa jamii nzima, ujenzi wa mabweni katika Sekondari za kata na Uchagiaji wa chakula kwa wazazi ili watoto wapate lishe.” Baadhi yao hutembea kilomita 10 hadi 20 kila siku, wakikumbana na uchovu, njaa na vishawishi vingi njiani.
(f) Mzazi mmoja kutoka Iramba, Singida, Joyce Lufega, mkazi wa Kijiji cha Lunsanga, katika Kata ya Mtenkente ward, anakiri kwamba alimshawishi binti yake aolewe mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, ili apate mahari ya shilingi 100,000/-. Anasema: “Nilimlazimisha binti yangu aolewe, lakini ndoa yenyewe ilidumu kwa miaka minne tu, kwa sababu msichana alikuwa bado mchanga mno hajastahili kuhimili majukumu ya kifamilia.”
(g) Mwathirika mwingine wa uamuzi wa wazazi kumharibia shule ili aolewe, ni Grace Ezekiel (26), mkazi wa Kijiji cha Kisiriri, Kata ya Kisiriri. Anasema mara alipohitimu elimu ya msingi, alinyimwa fursa ya kuendelea na sekondari mwaka 2002: “Nilikaa nyumbani kwa miaka mitatu, baadaye nikalazimishwa niolewe mwaka 2006. Wazazi wangu walipokea mahari ya shilingi 200,000/-.”
(h) Katika Wilaya ya Karatu, Manyara takwimu zinaonyesha kwamba katika Kata ya Endamarariek mwaka 2012 pekee, wanafunzi wa kike 14 wameripotiwa kupata mimba katika serikali za shule za kutwa. Mtendaji wa Kata ya Endamarariek, Omari Mshana, anasema: “Changamoto kubwa tunayokumbana nayo ni ushirikiano mdogo kutoka kwa wanafunzi na wazazi wenyewe. Inatuwia vigumu kuwachukulia hatua wahusika kwani mara nyingi mabinti hawa huhamishiwa sehemu nyingine mara tu anapopata mimba. Mara nyingi wanafunzi hawa hushurutishwa na wazazi wao kutowataja wanaume waliowapatia mimba na hivyo kudanganya kwamba wamepatiwa mimba wakiwa safari na watu wasiowajua.”
Naye Mtendaji wa Kata ya Rhotia, Jackson Sulle, anasema: “Tumepokea kesi saba za mabinti waliopewa mimba mwaka huu lakini wote wametoroshwa kupelekwa sehemu zisizofahamika.”
(h) Katika Wilaya ya Simanjiro, yapo matukio ambayo hutokanana watoto wenyewe kujiachia wapate mimba ili wafukuzwe shule. Ofisa Elimu ya Msingi wa Wilaya, Jackison Mbise, anasema kuachishwa shule kuna sura ya mimba na utoro: “Unaweza kukuta kati ya wanafunzi 194 wanaoanza shule, wanakuja kumaliza kati ya 40, 70 ama 100, wengine wanatoweka kwa njia kama hizi, wengi wa hawa wanaoacha shule ni wasichana, ingawa na wanaume kwa uchache wapo na wao huenda kuchunga Ng’ombe.”
7.0 UKEKETAJI
Ukeketaji uliripotiwa katika maeneo kadhaa, kwa kuwa hii ni mila ya makabila fulani nchini. Katika baadhi ya wilaya, kwa mfano Kilolo, mkoani Iringa, hakuna tatizo la ukeketaji. Katika sehemu nyingi za Jiji la Dar es Salaam, utafiti haukubaini ukeketaji. Hata hivyo, imebainika kuwa ukeketaji upo katika Kata ya Kitunda, kwa sababu wengi wa wakazi wake ni jamii ya watu kutoka Mkoa wa Mara, hasa Wakurya ambao moja ya mila na desturi zao ni kukeketa watoto wa kike. Lakini kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Renatus Ruhungu, ukeketaji umepungua sana kutokana na jitihada za wanaharakati na serikali kuelimisha umma na kuupiga vita.
Vile vile, utafiti umeshindwa kuthibitisha matukio ya ukeketaji katika Wilaya ya Handeni, Tanga; na Rungwe, mkoani Mbeya. Hata hivyo, jamii za mikoa kadhaa bado zinaendelea na mila ya ukeketaji, ingawa kwa kiwango kidogo.
7.1.0 Visa Mikasa
(a) Kuna dalili kwamba kasi ya ukeketaji imepungua katika Wilaya ya Karatu, lakini taarifa zinasema ukeketaji unafanywa kwa siri, kama anavyosema Mratibu wa Kata ya Karatu, Langew Ama: “Ukeketaji hufanywa katika maeneo ya vijijini ambapo watoto wachanga hukeketwa kwa siri pasipo kuwepo na sherehe za kimila ambazo kwa zamani ilikua ni lazima kwa zoezi kama hilo.”
(b) Katika Wilaya ya Kondoa, Dodoma, ukeketaji bado unafanyika lakini kwa kiwango cha chini, kutokana na ushawishi uliofanywa na wanaharakati. Sophia Seleman mkazi wa Kijiji cha Muluwa, Kata ya Suruke, anasema dhana ya ukeketaji ililenga kumfanya mwanamke asiwe na tamaa za kimwili. Anasema: “Siku hizi ni tofauti sana, kwani hapo zamani mwanamke asiyekeketwa alionekana ni malaya pia hakuweza kuheshimiwa wala kuthaminiwa yaani hakuweza kufanya chochote mbele ya wenzake, hata mwanangu amekeketwa. Sherehe za kuwatoa waliokeketwa ni maarufu kama ‘Lofumiavare,’ sherehe hizi zilifanyika wakati wa kuwatoa nje mabinti waliokeketwa, ambapo watu walikula na kunywa pamoja na kucheza, pia baadhi ya mabinti waliolewa kupitia sherehe hizi, na wengine waliambulia kubebeshwa mimba na wanaume wanaohudhuria sherehe hizo kwani hufanyika usiku.” Lakini Mwenyekiti wa Kijiji cha Tugufu, Kata ya Suruke, Yahaya Mohammed, anasema: “Kwa sasa yanafanyika kwa kificho kwani wazazi wanaweza kumuhamisha mtoto wanayetaka kumkeketa kutoka kata moja kwenda nyingine na wengine hudiriki kuwakeketa wakiwa wachanga.”
Hali ni ile ile katika Wilaya ya Same, mkoa wa Kilimanjaro. Vitendo vya ukeketaji vinafanywa kwa siri sana. Kwa Kipare kukeketa kunaitwa “kutavana;” na Wamasai wanasema “emorata.” Watoto wa kike wakishakua wakubwa, husubiriwa kipindi cha kufunga shule ndipo huchanganywa na watoto wa kiume waliotoka jando na kufanyiwa sherehe ya pamoja kugopa kugundulika kuwa wamekeketa watoto wao. Lakini Mwenyekiti Kijiji Darajani, Tatu Mkumbwa, anasema: “Wanajificha sana. Huwezi kusikia suala la ukeketaji siku hizi, lakini utamgundua mtoto wakati wa sherehe zao. Wanasema mtoto wa kike asipokeketwa hata akifikisha umri wa miaka 30 anaonekana mtoto mbele ya wenzake waliokeketwa, na hawezi kutoa uamuzi au ushauri akasikilizwa. Usipokeketwa huwezi kuingia unyago, kwa hiyo kimila ni lazima ukeketwe; lakini inafanyika kwa siri.”
(c) Wilayani Simanjiro ambakoo asilimia 95 ya wakazi wake ni Wamasai na Waarusha, ukeketaji unaendelea kwa kiwango kikubwa, ingwa wakeketaji wameacha kukeketa wasichana wakubwa (miaka 14-18). Badala yake wanakeketa watoto wadogo wenye umri wa wiki moja hadi mwezi mmoja.
Nang’urutu Kariayi (49), mkazi wa Narokusoito kata ya Langai, ni ngariba maarufu katika eneo hilo ambaye alianza kazi yake hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita. Anasema wanalinda mila zao, lakini wanakwepa kukamatwa. “Kwa siku nakata (nakeketa) hata zaidi ya watoto 10 kwa sababu mtu mmoja anaweza akawa ana mabinti watano; na ile kitu siyo ngumu kwa sababu haina mfupa,” anasema Kariayi.
(d) Moja ya wilaya za mfano ni Iramba, mkoani Singida. Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa wialaya hiyo, Hezron Msule, ukeketaji umekoma tangu mwaka 2005. Anasema mwaka huo ngariba wapatao 50 walikabidhi zama zao za kukuketea, baada ya kazi kubwa za wanaharakati na serikali kupinga ukeketaji na kuelimisha jamii juu ya madhara yake. Anasema: “Kampeni ilidumu kwa miaka mitano, 2000 hadi 2005, na yalikuwa mafanikio makubwa, kwani wasichana na wanawake hawakeketwi tena.” Hata hivyo, anadai bado kuna watu wachache wanaoendelea kuthamini mila hiyo, hasa wahamiaji kutoka maeneo jirani, wakiwamo Wanyaturu, lakini wanakabiliwa na doria za jeshi la polisi ambalo lilikabidhiwa jukumu la kudhibiti vitendo vya ukeketaji.
(e) Katika Wilaya ya Karatu, ukeketaji unaendelea kufanyika kwa siri. Nao wanakeketa watoto wachanga. “Ukeketaji hufanywa katika maeneo ya vijijini ambapo watoto wachanga hukeketwa kwa siri pasipo kuwepo na sherehe za kimila ambazo kwa zamani ilikua ni lazima kwa zoezi kama hilo,” anasema Langew Ama wa Rhotia Kati. Anasema miongoni mwa Wairaq, mila hiyo imepungua. Anasema: “Kama ukeketaji upo ni kwa kiwango kidogo sana, tena kwa maeneo ya vijijini ambapo hufanywa kwa siri kubwa pasipo serikali kujua.”
8.0 KIPIGO KWA WANAWAKE
Vipigo kwa wanawake ni jambo lililojitokeza kila mahali. Ni tatizo kubwa la kitaifa. Katika familia nyingi, wanawake bado wanaendelea kupigwa na wanaume, hasa waume zao au wapenzi wao. Lakini wengine wanapigwa pia na viongozi wa kiserikali. Miongoni mwa sababu za wanawake kupigwa ni ulevi, “mdomo” wa akina mama, ubabe wa akinababa, fumanizi, mfumo dume, ukiukwaji wa mafunzo ya ndoa, wivu, umaskini, “mapenzi,” ndoa za mitala, ndoa za kulazimishwa nk. Sheria dhidi ya kipigo, Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 ya mwaka 2002 kifungu 240 cha kinasema kwamba mtu yeyote aliyempiga mwenzake atakuwa ametenda kosa la jinai na atahukumiwa kwenda jela kwa muda wa mwaka mmoja.
Adhabu hii itatumika katika mzingira ambayo muathirika wa kipigo hakupata madhara makubwa sana. Aidha kifungu 241 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela kwa mtu yeyote aliyemdhuru mwenzake kwa kipigo na mtu huyo kupata madhara makubwa sana.

8.0.1 Visa Mikasa

(a) Katika Wilaya ya Temeke, Dar e salaam, mwaka 2011 kesi 14 ziliripotiwa. Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Mbagala (PPCM) Fatuma Katunzi, anasema kesi za vipigo zipo na kwamba mwaka 2011 zilifikishwa kesi 6, kati ya kesi hizo 2 zilitolewa hukumu ya kifungo na faini. Mwenyekiti wa Mtaa wa Msufini Kata ya Chamazi, Muharami Mlawa, anasema kesi 5 ziliripotiwa katika mtaa huo. Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Majimatitu ‘B’ Kata ya Charambe Fadhil Mpinga anasema kesi 3 za vipigo zilifikishwa kwake. Ofisa Mtendaji Mtaa wa Mianzini Jimmy Berege, anasema uongozi wa mtaa huo ulipokea kesi 6 kati ya kesi hizo tatu ziko polisi.
(b) Katika Wilaya ya Simanajiro, Neema Lalashe (46) mkazi wa Kijiji cha Uhuru katika Kata ya Orukasment, anasema kuwa kwa sasa vitendo hivyo vinafanyika kistaarabu tofauti na miaka ya nyuma. Anasema: “Zamani mwanaume alikuwa anafunga mikono na miguu kwenye mti ndiyo unachapwa, unapigwa mpaka unapoteza fahamu lakini siku hizi kidogo hayo mambo yamepungua, kama umekosea atakuchapa lakini hufungwi tena na kamba.” Naye Babu Mollel (73), anasema: “Sisi zamani ulikuwa unaoa mke siyo kwa sababu unampenda, lakini ni kwa sababu huko unapooa labda hiyo familia ni maarufu na umaarufu wa huku ni kuwa na ng’ombe wengi.”
(c) Kutoka Iramba, Singida, Wandoa Edward (37) mkazi wa Kijiji cha Kisiriri, Kata ya Kisiriri, anasema: “Nataka kurudu nyumbani, kwani nimechoka kuishi katika ndoa yenye manyanyaso. Nyumba yangu si salama tena.”
(d) Wilayani Karatu, vipigo dhidi ya wanawake vipo, ingawa ni nadra kwa matukio haya kuripotiwa katika vyombo vya dola. Mtendaji wa Kata ya Karatu, Paulo Lagwen anakiri kuwepo kwa vipigo kwa wanawake kutoka kwa waume zao. “Hata hivyo, idadi ya vipigo imepungua ikilinganishwa na zaman. Wanaume wa Kiiraq wamestaarabika kidogo kwa sasa. Idadi ya vipigo imepungua ikilinganishwa na zaman. Wanaume wa Kiiraq wamestaarabika kidogo kwa sasa,” anasema.
(e) Mkoani Mbeya, zipo ndoa nyingi zilizovunjika kutokana na kipigo kwa wanawake. Watu wote 22 waliohojiwa walikiri wanaume kuwepo kwa vipigo kwa wanawake. Mkazi wa kijiji cha Mpandapanda, Lucia Gwamaka, anasema kupigwa kwa mwanamke ni jambo la kawaida. “Ndiyo tunapigwa na wanaume, lakini inakuwa vigumu kumpeleka polisi. Kwanza nawaza watoto wangu, nikimpeleka polisi nitarudi wapi?” Anahoji.
f) Wilayani Kilolo mkoani Iringa ilibainika kuwa viongozi wanapofikishwa kwenye ofisi za kijiji kwa shitaka lolote viongozi wanajichukulia sheria mkononi na kuwapiga watuhumiwa. Kwa mfano utafiti ulishuhudia kisa mkasa ambacho wanawake wawili wajawazito katika Kijiji cha Kidabaga kwa nyakati tofauti walipigwa na viongozi wa kijiji hicho na hatimaye mimba walizokuwa wamebeba zikaharibika kutokana na madhara ya vipigo hivyo.Viongozi waliohusika na vipigo hivyo ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kidabaga, Nicolous Katandasi na Mtendaji wa kijiji hicho , Vincent Gaifalo .Kwa mujibu wa wanakijiji wa Kidabaga, mwenyekiti wa kijiji Nicolous Katandasi mnamo mwezi Mei 2011 alimtandika viboko vya nguvu 16 mama Silivia Kimata kitendo kilichosababisha mimba ya miezi mine ya yama huyo kuharibika. Aidha katika mwaka huu mtendaji wa kijiji hicho cha Kidabaga, Vincent Gaifalo alimchapa viboko 30 Seidina Kidwangise aliyefika kijijini hapo kumzika ndugu yake na kusababisha mimba yake kutoka na mama huyo kupata ulemavu wa kushindwa kusimama na kutembea. Mganga Mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Iringa dakta Deogratias Manyama alithibitisha kwamba hospitali hiyo mnamo tarehe 19 Aprili 2012 ilimpokea na kumlaza Seidina Kidwangise akiwa hawezi kusimama wala kutembea na uchunguzi ulikuwa umebainisha kuwa alikuwa amepoteza ujauzito na mwili wake ulikuwa na majeraha. Jambo la kushangaza wanakijiji hao walisema kuwa ingawa mtendaji wa kijiji aliyempiga mama huyo na kumsababishia madhara hayo makubwa alikuwa amefikishwa polisi, hawaamini kuwa haki itatendeka dhidi yake kutokana na kushamiri kwa rushwa hapo kijijini na kwenye vyombo vya sheria wilayani. “Ingawa wanakijiji wa Kidabaga wamechukua hatua na kuhakikisha kuwa viongozi hao wameondoka madarakani lakini hawajafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuumiza wanawake na kuharibu ujauzito wao”, alisema mwanakijiji mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuhofia maisha yake.
(g) Akina mama wa Kimasai wanapigwa lakini mila zao haziruhusu kushitaki. “Hata kama ameumizwa hawezi kusema badala yake huchinjiwa kondoo na kupewa mafuta kama tiba,” anasema Lea Saitobiki, Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji. Anasema hata kama utasikia amepigwa ukienda kumuuliza anakataa kata kata kuwa amepigwa.
Kufuatia masuala hayo kufanywa siri, hakuna takwimu zinazoonyesha tatizo la vipigo kwa wanawake lina ukubwa gani katika kata hiyo. Hata hivyo, kutokana na mahojiano na baadhi ya wananchi tatizo hilo linaonekana kuwepo kwa kiasi kikubwa, na mara nyingi linasababishwa na ugomvi wa kifamilia ambao hata hivyo, waathirika hawaripoti.
“Sisi kama serikali tunashindwa kuingilia mambo ya kifamilia, huwezi kwenda kwenye nyumba ya mtu ukaanza kuuliza wewe kwa nini unampiga mke wako wakati mke mwenyewe hajawahi kuja kuripoti,” anasema Afisa Mtendaji. Utafiti umebaini katika kata zingine zilizofanyiwa utafiti kuwa vitendo vya wanawake kupigwa hakuna takwimu kutokana na suala hilo kutoripotiwa kwenye ofisi za watendaji kata. “Haya mambo ya kupigana huwa wanayamaliza wenyewe nyumbani kwao, wakishindwa ndio wanakuja huku kwetu kushitakiana,” anasema Kaimu Afisa Mtendaji Kata ya Mwembe, Athumani Mkumbwa.
9.0 WANAWAKE NA WATOTO KUTELEKEZWA
Wanaume kutelekeza wake zao na watoto ni moja ya matukio ya kila mara katika maeneo yote ya utafiti. Utafiti huu umeonyesha kuwa sababu z kipigo kwa wanawake zinafanana na zina uhusiano na sababu zinazowafanya wanaume watelekeze wanawake. Miongoni mwa sababu hizo ni kukosa uaminifu, ugomvi usioisha, na maisha magumu. Imegundulika pia kuwa baadhi ya wanaume wanaotelekeza wake zao ni wale ambao hufanya hivyo kama njia ya kuepuka kuwapiga, kuwaumiza au kuwaua.
9.0.1 Visa Mikasa
(a) Zawadi Gwando ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Handeni, anasema malalamiko ya utelekezaji familia ni mengi eneo hilo. Anasema kwa siku nzima unaweza kupokea malalamiko yote ya utelekezaji mke na watoto katika mtizamo tofauti- wapo waliozalishwa kisha mwanaume kumtelekeza pamoja na mtoto ama mke kabisa wa ndoa kutelekezwa na watoto wake. Bi. Gwando anasema kila siku hupokea hadi kesi tatu za utelekezaji familia kutoka maeneo mbalimbali ya mji huo. “Vitendo vya utelekezaji familia vipo vingi, kwa kutwa unaweza kushinda ukipokea kesi za utelekezaji familia tu hadi mwisho wa kazi. Asilimia kubwa ya kesi za utelekezaji mke na watoto wanazopokea ni kutoka dini ya Kiislamu. Tatizo asilimia kubwa ya wakazi wa mji huu ni Waislamu ambao unakuta wana wake zaidi ya mmoja…sasa unakuta mume anatelekeza baada ya kuona hali ngumu ya maisha. Kwa upande wa Wakristu katika kesi 10 unaweza kumpata mmoja,” anasema Bi. Gwando.
(b) Wilayani Kondoa, Kaimu Mtendaji wa kata ya Suruke Jabir Issa Isere anasema athari za tatizo hili ni kubwa hasa kwa wanafunzi ambao hutelekezwa baada ya kupata mimba, hivyo pindi wanapojifungua huwaacha watoto wakilelewa kwa babu na bibi zao na wenyewe kukimbilia mijini kwa lengo la kujitafutia maisha. “Watoto na wanawake wanatelekezwa kila mara,kwani kila fedha inapopatikana katika familia nyingi badala ya kujadili ni nini kifanyike kujikomboa pale walipo wanaume huishia kutafuta mke wa pili na nyumba ndogo,” anasema. Naye Halima Mnjalo (20) Mkazi Kijiji cha Bolisa, anasema wanaume hutumia kisingizio cha kutafuta maisha na kuitelekeza familia. Anasema: “Mimi nilipata mimba nikiwa shuleni tangu mwanaume aliyenipa mimba hiyo alipofutwa aliondoka bila kuniaga wala sifahamu alipo kwani hatuna mawasiliano, hivyo jukumu la kumlea mtoto ni langu mwenyewe.”
(c) Wilayani Simanjiro, utelekezwaji unafanyika kwa wanaume kuondoka majumbani kwao na kuwaacha wanawake wakiendesha familia mbazo ni kubwa ama kuendelea kuishi nao lakini shughuli zote za familia wakiachiwa wao. Ana Moreta (49) mkazi wa Kijiji cha Narokusoito kata ya Langai ana mzigo wa kuendesha familia yenye watoto wanane baada ya mume wake kuondoka nyumbani na kwenda kusikojulikana. Kutokana na kutokuwa na mashamba wala mifugo, kwa sasa mama huyo analazimika kuendesha familia yake kwa biashara ya kuuza ugoro na maziwa kidogo anayoyauza baada ya kukamua ngombe wake wawili. Anasema kuwa, mume wake alitoweka nyumbani miaka tisa iliyopita na kwenda kusikojulikana.
“Mimi na mke mwenzangu tuko kwenye boma la mume wetu lakini hatujui alipo, yeye aliondoka tu hatujui alienda wapi,” anasema. Mama huyu anasema kuwa, baada ya kuona maisha yanazidi kuwa magumu, aliamua kwenda nyumbani kwao kuomba ng’ombe wawili anaowakamua kwa sasa.
(d) Kutoka Kilolo, Iringa, Ofisa Ustawi wa Jamii wa wilaya, Piencia Mushi, anasema: “Kuhama kwa wanaume kwenda mijini, nchi za jirani ikiwemo Msumbiji, kwenye mashamba makubwa ya mbao kufanya vibarua imekuwa ni moja ya sababu ya kutelekeza wanawake na watoto.”
(e) Kutoka Mvomero, Mkazi wa Kijiji cha Kidudwe, Kata ya Mtibwa, ambaye ni mwathirika wa kutelekezwa, Ester God, anasema katika miaka 10 alioishi na mumewe, ametelekezwa mara tatu. Mara ya mwiho jambo hilo lilimtokea akiwa na mtoto wa mwezi mmoja. “Baada ya kunitoroka na kuniacha na kichanga cha mwezi mmoja, nilijizoazoa na kuanza kuuza mboga ili kuwezesha watoto wangu wengine waendelee na shule na kupata chakula,” anasema.
(f) Wilayani Tarime, Mara, mkazi wa kijiji cha Korotambe, Christina Kyangwi, anasema mila ya Kikurya humruhusu mwanamume kuoa wanawake zaidi ya watatu. “Sasa kama kipato cha mwanamume ni kidogo, hulazimika kuikimbia familia yake moja na kuhamia kwenye familia yake nyingine, na tabia huendelea nayo na hatimaye kuondoka kabisa kijijini hapo.” Anasema kwamba kitendo cha kutelekezwa na mume wake na kuachwa na watoto wake wawili, kimemuathiri sana kisaikolojia na kumsababishia kupata maradhi ya moyo ambayo sasa yanamsumbua mara kwa mara. Kutokana na hali yake ya maisha kuwa duni, anashindwa kuwalea vizuri watoto wake kwani malezi mazuri hutokana na baba na mama wawapo pamoja. Akielezea athari nyingine, alisema ni rahisi sana kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwani itamsababishia kutafuta mwanamume mwingine wa kumpatia riziki ili kujikimu kimaisha.
10.0 HITIMISHO
Utafiti huu umedhihirisha kuwa unyanyasaji wa kijinsia ni ya maisha ya Watanzania. Wanawake na wasichana wengi wanafanyiwa vitendo vya kikatili na hawatoi taarifa popote kwa hofu ya kupata aibu au kutengwa na jamii. Baadhi ya sheria zilizopo hazikidhi matakwa, na nyingine zinakinzana. Vile vile, uelewa wa jamii kuhusu haki zao na wajibu wao na serikali ni mdogo. Umaskini unaendelea kuwa kisingizio cha unyanyasaji, hasa vijijini. Kwa sababu hiyo, watunga sheria na viongozi husika katika jami wanawajibika kuongoza harakati za kuondoa mazingira haya mabaya yanayodunisha maisha ya wananchi, hasa wanawake na watoto. Serikali inapaswa kuboresha mazingira vijijini, ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu mbadala ili kuondoa kero zinazosababisha uduni wa maisha unaotumiwa kuendeleza unyanyasaji wa kijinsia.
Lakini zaidi taasisi za umma na za kijamii zinapaswa kubuni mipango itakayoweza kuhamasisha umma kuacha kunyanyapaa waliofanyiwa ukatili kama vile kubakwa. Aidha wanapashwa kuchukua hatua kuhakikisha wanaotuhumiwa kwa makosa ya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji wananchi wanachukua jukumu la kumsaidia kupata na kutunza ushahidi na hatua za kisheria kuchukua mkondo wake.
Matokeo ya utafiti huu yatasaidia katika kuwafanya viongozi wa siasa na watendaji wa Serikali kupima kile walichofanya kama kimesaidia kumaliza matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yao. Taarifa kwamba viongozi hao hufumbia macho suala la ukeketaji, zitasaidia kuvipa vyombo vingine njia za kuwafuatilia na kuwawajibisha viongozi wazembe. Pia taarifa za kukuketwa kwa watoto wadogo, zinatoa fursa kwa wadau wa sekta ya afya na jinsia kufanya uchunguzi juu ya hali hii na kubuni njia mbadala za kuzuia unyanyasaji huu.
Ni dhahiri kwamba athari za unyanyasaji huu ni nyingi na za hatari, hasa kwa kizazi kijacho. Hivyo, ni vema serikali ichukulie kwa uzito wa pekee taarifa ili kuandaa mikakati ya kunusuru taifa kutoka kwenye unyanyasaji huu ambao unaweza kukatisha maisha ya baadhi ya wanajamii, na kudunisha maendeleo ya jamii huko tuendako.
Wazazi na viongozi wa jamii, hasa wa dini, wana jukumu la kuongeza nguvu katika kutoa malezi bora na mafundisho mwanana ya kiimani, kama njia ya kutokomeza tabia zitokanazo na mazoea mabaya na ukosefu wa uadilifu.

HII NDIO NEMBO MAALUM AMBAYO HUTUMIKA KATIKA KAZI MBALIMBALI ZA MABARAZA YA WATOTO NCHI TANZANIA BARA NA VISIWANI.

Thursday, January 24, 2013

NAFASI YA VYOMBO VYA HABARI

Waandishi wa Habari nchini Tanzania watakiwa kusimamia na kueleza haki za watoto pendekezo ambalo limetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Watoto UNICEF na kutaka afya, elimu na masuala ya kijamii yatiliwe mkazo zaidi. Hili limekuja kutokana na waandishi wengi kutojikita kueleza haki za watoto.

MAONI YA WATOTO KATIKA KATIBA MPYA





Maoni yameandaliwa na Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania



Tarehe: 22 Septemba 2012 na 8 Desemba 2012






Utangulizi
Baraza la watoto ni chombo huru cha uwakilishi wa watoto kilichoundwa hapa nchini mwaka 2002 na watoto wenyewe chini ya usimamizi wa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto kwa kufuata maelekezo yaliyoko kwenye Sera  ya Maendeleo ya mtoto ya mwaka 1996 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008 . Hadi kufikia  sasa serikali kwa kushirikiana na wahisani imeunda  mabaraza ya wilaya 87 .  Lengo kuu la kuanzisha Baraza la Watoto ni kuhakikisha  kunakuwepo na ulinzi wa haki  za watoto, ufuatiliaji na kutoa taarifa za uvunjwaji wa haki za watoto  nchini na kuhimiza wajibu wa mtoto.
Tunapenda kutoa Shukurani zetu za dhati kwa Mh. Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuteua na kuunda tume ya kukusanya maoni ya Katiba, pia tunaishukuru Tume hii kwa kutupa nafasi ya kutoa maoni.
Tunatambua serikali imekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia masuala ya watoto  ikiwemo kuingiza haki za binadamu kwenye katiba mwaka 1984 na kuanzisha sheria ya mtoto mwaka 2009,  sheria  na sera mbali mbali zinazowagusa watoto.

MAMBO MUHIMU AMBAYO WATOTO TUNAHITAJI YAWEMO KATIKA KATIBA MPYA.
1.HAKI NA WAJIBU WA MTOTO KUWEKWA KATIKA KATIBA
Katiba iliyopo haija onyesha wazi kuhusu upatikanaji wa haki za watoto, kwani katika sura ya kwanza sehemu ya tatu imezungumzia kwa ujumla kuhusu haki za binadamu. Kwa vile watoto ni zaidi 50% ya idadi ya Watanzania na wana mahitaji mengi ambayo yanatakiwa kupewa kipaumbele na taifa, hivyo tunaomba katiba mpya iweke kipengele kinachotamka wazi hasa katika nguzo kuu muhimu za haki za mtoto ambazo ni:

§  HAKI YA KUISHI, Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kupata chakula, matibabu, mavazi na kuishi kwenye mazingira safi,

§  HAKI YA KULINDWA, Katiba itamke wazi kwamba mtoto ana haki ya kulindwa na taasisi, mtu, jamii, familia na serikali dhidi ya matendo ya ubakaji, udhalilishaji, ukatili, ndoa za mapema, utumikishwaji katika kazi hatarishi,  mimba za utotoni, ukeketaji, kutoa mimba, matumizi ya dawa za kulevya, kuuzwa, kukoseshwa au kupoteza uraia,  vitendo vya ulawiti, kudhulumiwa mali, kutupwa au kutelekezwa na wazazi, kushirikishwa kwenye biashara ya ngono, kuonyeshwa picha za ngono,  mikataba - anapopewa ajira ambazo sio hatarishi mfano anaposhiriki kwenye matangazo yanayolenga kuelimisha jamii, kulindwa dhidi ya matangazo au habari za kutisha mfano picha za maiti na matangazo ya biashara yahusuyo ngono, mtoto alindwe na adhabu kali zinatolewa na jamii, familia na taasisi ambazo  zinapelekea kudhalilisha utu wake na kuhatarisha maisha yake. Mfano watoto kupewa adhabu ya kuchomwa moto, viboko, matumizi ya lugha chafu  zinazowadhalilisha watoto.

§  HAKI YA KUSHIRIKI, Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kushiriki kikamilifukatika kutoa mawazo au maoni katika mambo yanayohusu maisha yake au jamii na kulenga kuendeleza maisha yake. Pia katiba iweke msisitizo kuwa mawazo ya mtoto yaheshimiwe na yapewe uzito kulingana na upeo,umri na aina ya masuala anayoshirikishwa.

Katiba iweke msisitizo kuwa ushiriki wa mtoto uanzie ngazi ya familia, na maamuzi yote yanatolewa kwenye ngazi hii yalenge au yazingatie maslahi ya mtoto yaani yawe ya manufaa kwa mtoto. Katika hii haki ya kushiriki katiba itoe maelekezo kwa serikali kuweka mfumo ambao utamsaidia ushirikishwaji wa mtoto kwa kuanzisha mabaraza na mabunge ya watoto kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.

§  HAKI YA KUENDELEZWA, Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kuendelezwa kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii. Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kupata elimu kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, na itoe tamko kwa wizara husika kuweka mazingira bora yatakayomsaidia mtoto kusoma vizuri mfano vifaa vya kufundishia vya kutosha, walimu wa kutosha wenye ujuzi na upatikanaji wa chakula mashuleni

Katiba ionyeshe maadili ya mtoto na mtu mzima kuanzia miaka 18, mfano upendo, kudumisha amani, heshima, adabu umoja na ari ya kujitegemea na kuthamini kazi. Katiba ianishe adhabu zitakazotolewa kwa mtu yeyote atakayeenda kinyume na hayo maadili mfano kuvaa mavazi ya nusu uchi na kutamka matusi hadharani.

§  Haki ya Kutobaguliwa: Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kutobaguliwa kwa hali yoyote ile mfano kijinsi, hali ya kimaisha , ugonjwa, ulemavu, uyatima na jinsi anayvoonekana mbele za watu, dini, utaifa na utamaduni. Katiba iweke msisitizo kuwa watoto wanapokuwa wanapewa huduma ikiwemo ya elimu, afya,chakula na huduma zozote zile ambazo ni muhimu wanatakiwa wasibaguliwe.

Pamoja na haki nyingine zilizotajwa hapo katiba itamke pia na kuweka msisitizo kuwa mtoto ana haki ya kupata jina zuri kutoka kwa wazazi wake lisilolenga kumdhoofisha mtoto, pia itoe uhuru wa mtoto kubadili jina linalomdhoofisha na kusikia aibu ndani ya jamii.  Pia katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kupata  cheti cha kuzaliwa na kusajiliwa mara tu anapozaliwa

2. WAJIBU WA MTOTO
Mtoto ana haki pia ana wajibu, Katiba itamke wajibu wa mtoto kama ulivyoanisha kwenye sheria ya mtoto ya mwaka 2009, kuwa ni
·         Kufanya  Kazi kwa lengo la kuhimarisha umoja wa familia
·         Kuheshimu wazazi, walezi, wakubwa zake na wazee na kuwasaidia pale wanapohitaji msaada
·         Kusadia jamii na taifa lake kwa kutumia uwezo wake wote wa kimwili na kiakili kulingana na umri wake
·         Kutunza na kuhifadhi mila na desturi sahihi za jamii na taifa lake kama ilivyo kwa watanzania wengine.

Katiba itamke kuwa mtoto atakiwi kuvunjiwa haki yake kwa vile anatimiza wajibu ulioainishwa hapo juu.


        3. HAKI ZA WATOTO  WENYE ULEMAVU
Serikali itambue kuwa ulemavu unatofautiana, kwa hiyo na huduma zinazotolewa kwa makundi haya zitofautiane. Hivyo katiba itamke kuwa watoto wenye ulemavu wana haki za msingi kama watoto wengine mfano haki ya Kupata elimu, matibabu, mavazi, malazi,kushiriki, kupata jina zuri, chakula na ulinzi.

Katiba iweke msisistizo na kutamka kuwa watoto wenye ulemavu wa ngozi wanastahili kupata ulinzi maalumu, kuwa na shule maalumu ambazo ni za bweni na wanapokwenda kwenye mikusanyiko kama mikutano mikubwa wapewe ulinzi na vyombo vya usalama na pia anapokuwa mmoja mmoja apewe msaidizi. Pia katiba itoe tamko kuwa hawa watoto wenye ulemavu wapewa huduma kama vifaa vya kusomea na mafuta kwa ajili ngozi.
Watoto wenye ulemavu wa viungo wana haki ya kupata viungo bandia, baiskeli, elimu, huduma za afya na kuhakisha majengo yanayotoa huduma muhimu ni rafiki kwa walemavu.

Pia katiba itamke kuwa  watoto wenye ulemavu wa macho, wanahitaji vifaa vya kusomea, maandishi ya nukta nundu, fimbo za kutembelea, walimu wa kutosha wenye utaalamu wa kuwafundisha watoto hao.
Pia katiba izungumzie kuwa watoto wenye ulemavu wa kutosikia wanahitaji  walimu wenye ujuzi katika mafunzo ya lugha za ishara.  

4.MABARAZA YA WATOTO YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUTAMBULIKA KIKATIBA.
Tunapendekeza katiba mpya iweke kipengele cha kutambua mabaraza ya watoto na kutoa maelekezo kwa serikali kuanzisha mabaraza kuanzia ngazi ya mtaa/ kijiji hadi taifa na kutenga rasilimali za kuendesha mabaraza hayo.  Hii itawapa nafasi watoto kukusanyika mahali pamoja, kushiriki na kutoa maoni juu ya masuala yanayowahusu ambayo ni haki yao kikatiba.

5. WATOTO KUWA  NA MBUNGE WAO WA KUWAWAKILISHA BUNGENI
Kwa kuwa watoto ni zaidi ya nusu ya idadi ya watanzania wote na wana mahitaji mengi yanayohitaji kupewa kipaumbele na taifa. Katiba mpya iweke mfumo wa wawakilishi wa watoto bungeni kwa kutoa nafasi 2 za wabunge mmoja kutoka Zanzibar na mmoja kutoka Tanzania Bara wa kuzungumzia masuala yanayowahusu watoto. Katiba itoe tamko kuwa wabunge hao (2) wateuliwe na Raisi kwa kuwashirikisha watoto wa Baraza la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

6. VYETI VYA KUZALIWA KWA WATOTO.
Kumekuwepo na tatizo kubwa la upatikanaji wa vyeti vya  kuzaliwa , na tatizo hili linatokana na baadhi ya wazazi kushindwa kupata fedha za kulipia gharama zilizowekwa kupata cheti cha kuzaliwa, pia sababu nyingine ni kwamba hizo huduma ziko mbali sana na wananchi  hali ambayo inapelekea usumbufu kwa wazazi kutembea umbali mrefu au kuingia gharama kufuata vyeti hivyo kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya.

Hivyo basi tunaomba katiba itamke watoto wote kuanzia umri wa miaka 0-17 badala ya miaka 0 - 5 wapatiwe vyeti bure bila mzazi kulipia gharama yeyote.
Pia tunaomba katiba itamke na kutoa mamlaka kwa vituo vya afya, zahanati na hospitali kutoa vyeti vya kuzaliwa.

7. MFUMO WA ELIMU.
Mfumo wa elimu uliopo sasa unaleta ubaguzi kati ya watoto wanaotoka kwenye familia zenye kipato kizuri na familia duni au maskini. Mfano watoto wanaosoma shule za binafsi au ‘English medium school’ wanafanya vizuri zaidi katika masomo hasa sekondari na wengi wao wanaotoka kwenye familia zenze kipato bora na wale wanaotoka familia duni au maskini wanasoma kwenye shule za kawaida ambapo elimu sio bora. Lugha inayotumika kufundishia ni tofauti, uwezo wa walimu ni tofauti na gharama zinazolipwa kwenye hizo shule ni kubwa ambapo mzazi wa kawaida hawezi kulipia

Kutokana na hali hii tunaomba Katiba itamke kuwa lugha ya kufundishia iwe ya kiingereza katika shule zote kuanzia awali, mitaala yote ya kufundishia iwe sawa na muda wa kubadilishia mtaala uwe mrefu angalau miaka 10 ili tuone matunda ya mitaala hiyo.  katiba itoe tamko kuwepo mfumo maalumu wa kitaifa wa kubadilisha  mitaala na mfumo huo uwashirikishe wadau wa elimu wakati wa kufanya marekebisho kwenye  mitaala.  Pia katiba itamke uwepo wa taasisi au bodi maalumu ya kuratibu gharama za uendeshaji wa shule za sekondari, misingi na elimu ya juu (vyuo vikuu)  

8.MFUMO WA HUDUMA ZA AFYA
Katiba mpya itamke wazi huduma za afya kwa watoto zitolewe bure kuanzia miaka 0 -17, na itoe maelekezo kwa serikali na sekta husika kuweka mifumo ambayo itasaidia huduma hizo kupatikana bure. Mfano  uchangiaji wa bima za afya ngazi ya kaya. Ili kuboresha afya ya mama na mtoto tunaomba katiba itamke kuwa mama anapojifungua apewe likizo ya miezi 6 ili aweze kumunyonyesha mtoto miezi 6 mfululizo bila kumpa chakula  chochote  tofauti na ilivyokuwa awali, hii itasaidia wanawake kupata muda mzuri wa kuwa karibu na kuwanyonyesha watoto wao kwa muda wa kutosha.

9.MASUALA YA MUUNGANO
Suala la elimu ya awali hadi sekondari liwe la muungano, kusiwepo utofauti wa mitaala kati ya Tanzania visiwani na Tanzania bara ili kuweka usawa katika ufahamu na uelewa wa watoto na taifa kwa ujumla.

10.SHERIA , SERA , MILA NA DESTURI ZINAZOVUNJA HAKI ZA WATOTO
Katiba mpya itamke wazi sheria, sera na taasisi zote zinazokiuka na kuvunja haki za watoto zifutwe. Kwa mfano sheria au sera ya elimu inayotamka kumfukuza mtoto wa kike anapopewa mimba wakati akiwa shuleni, imegundulika kwamba watoto wanaoachishwa shule au kufukuzwa shule kwa ajili ya mimba wanaishia mitaani, wengine wanaamua kuolewa wakiwa na umri mdogo mwisho wa siku tutakuwa na taifa lenye watoto wa kike wengi wasiokuwa na mwelekeo wa kimaisha au wasiokuwa na elimu. Kupata mimba kisiwe kigezo cha kumvunjia mtoto haki yake ya kusoma. Kutokana na hili suala tunapendekeza katiba iweke kipengele cha kufuta  sheria ya Elimu inayotamka kuwa mtoto wa kike akipata mimba afukuzwe shule na kurudisha nyumbani pia itoe tamko moja kwa moja kuwa mtoto akipewa mimba arudi shule, katiba itoe maelekezo ya kumrudisha mtoto shule nyingine ili aweze kuendelea na masomo.

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inapelekea watoto kuvunja haki zao kwa kuwa inamruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi na wakiume kuoa akiwa na umri wa miaka 18, kwa kuwa vitendo vya watoto wa kike kuolewa wakiwa wadogo vimekidhiri, taifa halihitaji tena kuwa na sheria hiyo kwani inakinzana na sheria nyingine kama vile sheria ya mtoto ya mwaka 2009  ambayo imeanisha umri wa mtoto na majukumu ya mtoto, pia inatoa ubaguzi na kuonekana inamkandamiza na kumbagua mtoto wa kike kwanini imruhusu mtoto wa kike kuolewa na umri wa miaka 15 na mtoto wa kiume kuoa akiwa na miaka 18. Pia kuendelea kuwepo kwa sheria hiyo kutawapa fursa wazazi kuendelea kuwaozesha mabinti zao badala ya kuwaendeleza kwa vile sheria inawalinda. Hivyo Basi tunapendekeza katiba ije na tamko la kuwa umri wa kuolewa au kuoa ni miaka 18 na itoe tamko la kufutwa sheria ya ndoa kama itakuwa haijabadili kipengele hicho ndani ya mwaka mmoja tangu kutungwa kwa katiba.

Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka1998, watoto tunatambua kuwa kuna marekebisho madogo yaliyofanywa kwenye sheria hiyo baada ya kutungwa kwa sheria ya mtoto mwaka 2009 hasa kwenye adhabu kwa mtoto aliyefanya kosa la kujamiiana mtoto mwenzake. Ila kipengele kinachotamka kuwa mtu hatahesabika amembaka msichana mwenye umri wa miaka 15 ikiwa amejamiiana naye wakiwa katika ndoa ambayo wazazi wameridhia hakikufanyiwa marekebisho kipengele hiki kinaendelea kulinda kile kipengele kilicho kwenye sheria ya ndoa kinachomruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15 kuolewa. Tunaomba katiba itamke kufutiliwa mbali kipengele hicho kwani kinaendelea kunyima haki mtoto kwa kumshirikisha kwenye vitendo vya ngono akiwa mdogo.

Sheria na miongozo ya Elimu iliyopo kwa ajili ya matumizi ya adhabu ya viboko mashuleni. Suala adhabu ya viboko mashuleni zimekithiri na walimu wanatoa adhabu ya viboko bila miongozo iliyopo hadi kufikia watoto kuchapwa bila kufahamu kosa lake. Adhabu nyingine mbaya kwa watoto ni pamoja na watoto kuchimba mashimo, kung’oa visiki, kupiga magoti na kufyatua tofali.  Adhabu hizo zinamuathri mtoto kimwili na kisaikolojia   pia kumdhalilisha mtoto ambavyo ni kinyume na haki za mtoto zilizoainishwa kwenye sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa zinazozuia kumjeruhi mtoto kimwili, kumdhalilisha na kufanyiwa vitendo vya ukatili vyenye kumshusha utu na hadhi kwa mtoto. Hivyo tunaomba katiba itoe tamko la kufuta hiyo miongozo na sera hizo kwani zinatoa mwanya mkubwa kwa walimu kuendelea kuwanyanyasa watoto. Pia katiba itoe tamko kwa jamii kuacha mila au utamaduni zinazoleta madhara kwa mtoto, kwa mfano suala la viboko na adhabu kali zimeonekana pia zikitolewa na wanafamilia, na ni utaratibu umekuwepo kizazi hadi kizazi.

11. TUME YA TAIFA YA HAKI ZA WATOTO
Katiba mpya iunde tume huru ya kudumu ya taifa ya haki za mtoto yenye utaalamu wa kushughulikia haki za watoto ikiwa ni pamoja na kusimamia, kupokea taarifa,  kufuatilia uvunjwaji na kutoa mapendekezo juu ya hatua za kuchuliwa na serikali au taasisi dhidi ya ukiukwaji wa haki za mtoto. Pia itoe maelekezo ya uundwaji wa kamati mbali mbali zinazoshughulikia masuala ya watoto kuanzia ngazi ya mtaa/ kijiji hadi mkoa zitakazo fanya kazi kwa karibu na tume.

12.ULINZI WA WATOTO AMBAO HAWANA MAKAZI MAALUMU,NA WALE WAISHIO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI.
Katiba itoe tamko kuhusu utekelezwaji  wa mifumo ya ulinzi wa mtoto iliyoko nchini mfano ule mpango mkakati wa ulinzi wa mtoto kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa ya kushughulikia masuala ya watoto  waishio katika mazingira hatarishi au maelekezo  kwa serikali na sekta husika kuweka mfumo maalumu juu ya ulinzi wa watoto ambao hawana makazi maalumu na waishio katika mazingira hatarishi.

13.KUWEPO NA WIZARA YA WATOTO TU.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inayoshughulikia masuala ya watoto hivi sasa imeelemewa na mambo mengi na hata bajeti inayotengewa kwa ajili ya wizara hiyo haikidhi mahitaji ya watoto. Hivyo tunapendekeza katiba mpya ije na tamko la kuunda wizara maalumu kwa ajili ya watoto kwani vile watoto ni sehemu kubwa sana ya watanzania wote kwani zaidi ya nusu ya watanzania ni watoto kwanini tuchanganywe na na wizara zingine?

HITIMISHO
Baraza la watoto linaahidi kushirikiana na tume katika mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba mpya.