Monday, December 31, 2012

Migogoro ya ndoa, malezi mabovu chanzo cha watoto wa mitaani


TATIZO la watoto wa mitaani limekithiri nchini  licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali, mashirika na watu binafsi.
Naandika makala haya baada ya kufanya uchunguzi binafsi kwa Jiji la Dar es Salaam nikifuatilia watoto hao.

Siyo siri kwamba ukifika Dar es Salaam hasa maeneo ya Kariakoo nyakati za usiku, utashangaa kuona watoto wengi wakiwa wamelala kwenye viambaza vya majengo mbalimbali.

Watoto hawa, mara nyingi hushinda wakiomba fedha barabarani mchana, wengine hufanya kazi ngumu kama vile kuosha magari, kubeba mizigo na wengine ni vibaka.
Siyo ajabu kuona watoto walio chini ya miaka 10 wakivuta sigara, bangi au gundi kilevi. Watoto hao hujifunza kila aina ya maisha, ambayo hawakustahili, lakini yote ni kutokana na kukosa mwongozo wa maisha kutoka kwa wazazi au jamii husika.
Watoto hawa hawana ulizi wowote na wanalala katika mazingira hatarishi, matokeo yake huishia kubakwa huku  wavulana  wakilawitiwa.
Tafiti nyingi zilizofanyika na nyingine zinaendelea kufanyika kuhusu tatizo hili, zinathibitisha kuwa migogoro katika ndoa na malezi mabovu ndiyo chanzo cha tatizo hilo.
Takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)  zinaonyesha kuwa, idadi ya watoto wanaoishi mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu wanakadiriwa kufikia 120 milioni duniani.
Miongoni mwa watoto hao, 30 milioni wako katika Bara la Afrika, Tanzania ikiwa moja kati ya nchi hizo yenye changamoto kubwa ya ongezeko la watoto wa mitaani kila kukicha.

Kwa mujibu wa UNICEF, katika Bara la Afrika, maelfu ya watoto wanateswa, kutumiwa vibaya pamoja na kufanyiwa ukatili.

Watoto 50 milioni kati ya hao ni yatima kwa sababu mbalimbali ikiwamo ugonjwa wa Ukimwi. 
 
Takwimu hizo zinaeleza kuwa zaidi ya theluthi moja ya watoto hao wana umri ulio kati ya miaka mitano hadi 14 na wanafanyishwa kazi ngumu. 



Mbali na takwimu hizo, Utafiti uliofanywa hapa nchini Agosti, mwaka 2009 na shirika lisilo la kiserikali la Uingereza “Consortium for Street Children,” ulibaini kuwapo idadi kubwa ya watoto wa mitaani.

Utafiti huo uliofanyika katika miji mikuu saba hapa nchini, umebaini sababu mbalimbali zinazochangia kuwapo kwa idadi hiyo, huku njaa na ukatili wa majumbani vikiongoza.

Miji hiyo ni Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida na Kilimanjaro ambapo utafiti ulibaini ongezeko kubwa la idadi ya watoto wanaoishi mitaani huku Jiji la Dar es Salaam likiongoza kwa kuwa  na watoto wengi wanaoishi mitaani.


Mbali na takwimu hizo, imebainika kuwa asilimia 50 ya watoto wanaoishi mitaani  pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu inatokana na ukatili unaofanywa majumbani dhidi ya watoto hao.

Pia asilimia 35 ya watoto hao wanaoishi mitaani, inatokana na watoto hao kuzikimbia familia zao  kutokana na njaa pamoja na umaskini uliokithiri.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani duniani kwa sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya 100 milioni.
Asilimia 70 hadi 80 ya watoto hawa husimulia kuwa wametoroka nyumbani baada ya familia kusambaratika. Asilimia  nne ya watoto hao wa mitaani hufanyiwa ukatili baada ya  kuvunjika kwa ndoa.
Licha ya kuwapo sheria zinazowalinda watoto juu ya ukatili, inaonekana kuwa sheria hizo bado hazijapewa kipaumbele kama sheria nyingine.
Hata hivyo, kabla ya kwenda kwenye sheria hizo, tuangalie vyanzo vya tatizo hilo.
Kama tafiti hizo zinavyoeleza, tatizo hilo ni kubwa, hivyo jitihada za kupambana nalo pia zinapaswa kuwa kubwa.
Tafiti hizo zinaonyesha kuwa migogoro kwenye familia ni chanzo kimojawapo cha watoto kukimbia familia na kwenda kuishi mitaani, kuna haja ya jamii kuliangalia upya suala la mahusiano ya kimapenzi, ambalo mwisho wake huzalisha familia kuwa bora au mbaya.
Tunaelewa kuwa suala la mapenzi mara nyingi linakuja kama ajali, ambapo watu wa jinsia mbili tofauti hutokea kupendana.
Hapo ndipo uhusiano huanza hadi kufikia watu kupata watoto. Lakini, ni wazi kuwa, suala la mapenzi na malezi ya watoto ni vitu viwili tofauti.
Mara nyingi vijana walio wengi wamejiingiza kwenye mapenzi bila kufahamiana vizuri na wenzi wao au bila hata kuwa na maandalizi ya kutosha ya kuwa na familia.
Matokeo yake mapenzi yanapokolea na watoto wakapatikana, wenzi wao hukimbia.
Wasichana wengi wamejikuta njia panda kwa kushindwa kulea watoto peke yao, hatimaye kuwaacha wakirandaranda mitaani na hao ndiyo wanaokimbilia mijini.
Nadhani hapa ndipo kuna haja pia ya kurudi kwenye mila na desturi zetu, ambapo kulikuwa na taratibu nzuri za kuwatafutia vijana wenzi.
Wazazi wa pande mbili walimtafutia kijana wa kiume mchumba walioyemfahamu vizuri.
Hata tatizo linapotokea, wazazi au walezi huwa na kazi rahisi ya kufuatilia na kutatua tatizo.
Hata hivyo, kwa mtindo wa sasa wa utandawazi inakuwa vigumu kutatua tatizo linapotokea.
Vijana wanajichukulia tu wasichana na ‘kuwatundika mimba’ kisha kukimbia. Wasichana pia hujipeleka tu kwa wavulana ambapo hubebeshwa mimba na kuachwa njia panda. Hii ni dalili ya ukosefu wa maadili katika jamii.
Tatizo jingine ni migogoro ya ndoa, ambayo mara nyingi husababishwa na wanandoa kutokuwa waaminifu katika ndoa hizo.
Utakuta wanandoa wanapendana sana siku za mwanzo, wanapata watoto na maisha yanakwenda vizuri.
Mambo huaribika baadaye ambapo mmoja wa wanandoa huanza kuwa na mahusiano mengine nje ya ndoa.
Mara nyingi wanaume ndiyo hulaumiwa kwa hili, ingawa  wapo pia wanawake wasio waaminifu.
Utakuta mwanamume ananogewa na penzi la nje, hata kusahau majukumu yake katika familia.
Tukumbuke kwamba mama peke yake hawezi kufanya malezi ya watoto kikamilifu. Watoto pia wanahitaji malezi na upendo kutoka kwa baba.
Mara nyingi tatizo hilo linakwenda sanjari na ulevi wa kupindukia. Kwa hili, pia wanaume uhusishwa ambapo hutumia fedha wanazopata kwa ulevi kuliko kutunza familia.
Familia nyingi zimevurugika kutokanana na ulevi wa wanandoa.
Tabia ya ulevi pia inaendana na ugomvi kwa wanandoa. Utakuta wanandoa wanapigana hata mbele ya watoto, hivyo kuwahuzunisha na kuwakatisha tamaa wangali bado wadogo.
Ugomvi wa mara kwa mara ndiyo chanzo cha watoto wengi kukimbia familia.
Liko pia tatizo la ukatili kwa watoto. Si rahisi kwa mwanamke aliyemzaa mtoto wake amfanyie ukatili, ingawaje hutokea mara chache ambapo wapo wanawake hudiriki hata kutoa mimba au hata kuwatupa watoto waliowazaa.
Matatizo ya ndoa za mitala au watoto kulelewa na mama wa kambo au walezi wengine, huchangia kwa kiasi kikubwa pia kuwepo kwa ukatili kwa watoto.
Matatizo yote haya ndiyo yanasababisha watoto kukimbilia mitaani na kukumbana na matatizo yote hayo.
Kwa kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka, uwepo wa watoto wa mitaani ni janga jingine kwa taifa.
Kama watoto hawa watakuwa wakiongezeka kwa kiasi hiki itafika mahali kutakuwa kizazi cha watu wasio na elimu, ujuzi wala kazi za kujikimu. Hilo ni tishio kwa uchumi na maendeleo ya taifa kwa jumla.
Ni vyema sasa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto kurekebisha sheria zake na kutilia mkazo malezi bora kwa watoto.
Kuwe na ufuatiliaji wa karibu kwa familia zisizotoa malezi bora kwa watoto, ikiwezekana washtakiwe.
Kuna haja pia ya kuongeza vituo vya kulea watoto wa mitaani na Serikali itoe ruzuku kwa vituo hivi, ili kuviwezesha vituo hivyo kukabiliana na jukumu hilo.
Hata hivyo, wamiliki wa vituo hivyo nao wanapaswa kufanya kazi kwa moyo na siyo kutafuta masilahi pekee. Kuna malalamiko mengi kwamba wamiliki wa vituo hivyo wamekuwa wakijinufaisha binafsi na misaada inayotolewa kwa ajili ya watoto hao.
Kila mtu ana jukumu la kukabiliana na tatizo hili, hivyo kama ni wanandoa, tuhakikishe kwamba familia zetu zinakuwa bora badala ya kuvurugika.
Kwa wale ambao bado hawajaingia kwenye ndoa nao wanajukumu la kuhakikisha tatizo hilo haliendelei.

No comments:

Post a Comment