|
Maoni yameandaliwa na
Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
|
|
|
Tarehe: 22
Septemba 2012 na 8 Desemba 2012
|
|
Utangulizi
Baraza la watoto ni
chombo huru cha uwakilishi wa watoto kilichoundwa hapa nchini mwaka 2002 na
watoto wenyewe chini ya usimamizi wa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya
Jamii,Jinsia na Watoto kwa kufuata maelekezo yaliyoko kwenye Sera ya Maendeleo ya mtoto ya mwaka 1996 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2008 . Hadi kufikia
sasa serikali kwa kushirikiana na wahisani imeunda mabaraza ya wilaya 87 . Lengo kuu la kuanzisha Baraza la Watoto ni
kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi wa haki
za watoto, ufuatiliaji na kutoa taarifa
za uvunjwaji wa haki za watoto nchini na
kuhimiza wajibu wa mtoto.
Tunapenda kutoa Shukurani
zetu za dhati kwa Mh. Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuteua na
kuunda tume ya kukusanya maoni ya Katiba, pia tunaishukuru Tume hii kwa kutupa
nafasi ya kutoa maoni.
Tunatambua serikali
imekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia masuala ya watoto ikiwemo kuingiza haki za binadamu kwenye
katiba mwaka 1984 na kuanzisha sheria ya mtoto mwaka 2009, sheria
na sera mbali mbali zinazowagusa watoto.
MAMBO
MUHIMU AMBAYO WATOTO TUNAHITAJI YAWEMO KATIKA KATIBA MPYA.
1.HAKI
NA WAJIBU WA MTOTO KUWEKWA KATIKA KATIBA
Katiba iliyopo haija onyesha wazi kuhusu upatikanaji wa haki za watoto,
kwani katika sura ya kwanza sehemu ya tatu imezungumzia kwa ujumla kuhusu haki
za binadamu. Kwa vile watoto ni zaidi 50% ya idadi ya Watanzania na wana mahitaji
mengi ambayo yanatakiwa kupewa kipaumbele na taifa, hivyo tunaomba katiba mpya
iweke kipengele kinachotamka wazi hasa katika nguzo kuu muhimu za haki za mtoto
ambazo ni:
§ HAKI YA KUISHI, Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kupata chakula,
matibabu, mavazi na kuishi kwenye mazingira safi,
§ HAKI YA KULINDWA, Katiba itamke wazi kwamba mtoto ana haki ya kulindwa
na taasisi, mtu, jamii, familia na serikali dhidi ya matendo ya ubakaji,
udhalilishaji, ukatili, ndoa za mapema, utumikishwaji katika kazi hatarishi, mimba za utotoni, ukeketaji, kutoa mimba,
matumizi ya dawa za kulevya, kuuzwa, kukoseshwa au kupoteza uraia, vitendo vya ulawiti, kudhulumiwa mali,
kutupwa au kutelekezwa na wazazi, kushirikishwa kwenye biashara ya ngono,
kuonyeshwa picha za ngono, mikataba - anapopewa
ajira ambazo sio hatarishi mfano anaposhiriki kwenye matangazo yanayolenga
kuelimisha jamii, kulindwa dhidi ya matangazo au habari za kutisha mfano picha
za maiti na matangazo ya biashara yahusuyo ngono, mtoto alindwe na adhabu kali
zinatolewa na jamii, familia na taasisi ambazo
zinapelekea kudhalilisha utu wake na kuhatarisha maisha yake. Mfano
watoto kupewa adhabu ya kuchomwa moto, viboko, matumizi ya lugha chafu zinazowadhalilisha watoto.
§ HAKI YA KUSHIRIKI, Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kushiriki
kikamilifukatika kutoa mawazo au maoni katika mambo yanayohusu maisha yake au
jamii na kulenga kuendeleza maisha yake. Pia katiba iweke msisitizo kuwa mawazo
ya mtoto yaheshimiwe na yapewe uzito kulingana na upeo,umri na aina ya masuala
anayoshirikishwa.
Katiba iweke msisitizo kuwa ushiriki wa mtoto uanzie ngazi ya familia, na
maamuzi yote yanatolewa kwenye ngazi hii yalenge au yazingatie maslahi ya mtoto
yaani yawe ya manufaa kwa mtoto. Katika hii haki ya kushiriki katiba itoe
maelekezo kwa serikali kuweka mfumo ambao utamsaidia ushirikishwaji wa mtoto
kwa kuanzisha mabaraza na mabunge ya watoto kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.
§ HAKI YA KUENDELEZWA, Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kuendelezwa
kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii. Katiba itamke kuwa mtoto ana
haki ya kupata elimu kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, na itoe tamko
kwa wizara husika kuweka mazingira bora yatakayomsaidia mtoto kusoma vizuri
mfano vifaa vya kufundishia vya kutosha, walimu wa kutosha wenye ujuzi na upatikanaji
wa chakula mashuleni
Katiba ionyeshe maadili ya mtoto na mtu mzima kuanzia miaka 18, mfano
upendo, kudumisha amani, heshima, adabu umoja na ari ya kujitegemea na
kuthamini kazi. Katiba ianishe adhabu zitakazotolewa kwa mtu yeyote atakayeenda
kinyume na hayo maadili mfano kuvaa mavazi ya nusu uchi na kutamka matusi hadharani.
§ Haki ya Kutobaguliwa: Katiba itamke kuwa mtoto ana haki ya kutobaguliwa
kwa hali yoyote ile mfano kijinsi, hali ya kimaisha , ugonjwa, ulemavu, uyatima
na jinsi anayvoonekana mbele za watu, dini, utaifa na utamaduni. Katiba iweke
msisitizo kuwa watoto wanapokuwa wanapewa huduma ikiwemo ya elimu, afya,chakula
na huduma zozote zile ambazo ni muhimu wanatakiwa wasibaguliwe.
Pamoja na haki nyingine zilizotajwa hapo katiba itamke pia na kuweka
msisitizo kuwa mtoto ana haki ya kupata jina zuri kutoka kwa wazazi wake
lisilolenga kumdhoofisha mtoto, pia itoe uhuru wa mtoto kubadili jina linalomdhoofisha
na kusikia aibu ndani ya jamii. Pia katiba
itamke kuwa mtoto ana haki ya kupata
cheti cha kuzaliwa na kusajiliwa mara tu anapozaliwa
2. WAJIBU WA MTOTO
Mtoto ana haki pia ana wajibu, Katiba itamke wajibu wa mtoto kama
ulivyoanisha kwenye sheria ya mtoto ya mwaka 2009, kuwa ni
·
Kufanya Kazi
kwa lengo la kuhimarisha umoja wa familia
·
Kuheshimu wazazi, walezi, wakubwa zake na wazee na
kuwasaidia pale wanapohitaji msaada
·
Kusadia jamii na taifa lake kwa kutumia uwezo wake
wote wa kimwili na kiakili kulingana na umri wake
·
Kutunza na kuhifadhi mila na desturi sahihi za
jamii na taifa lake kama ilivyo kwa watanzania wengine.
Katiba itamke kuwa mtoto atakiwi kuvunjiwa haki yake kwa vile anatimiza
wajibu ulioainishwa hapo juu.
3. HAKI ZA WATOTO WENYE ULEMAVU
Serikali itambue kuwa ulemavu unatofautiana, kwa hiyo na huduma
zinazotolewa kwa makundi haya zitofautiane. Hivyo katiba itamke kuwa watoto
wenye ulemavu wana haki za msingi kama watoto wengine mfano haki ya Kupata
elimu, matibabu, mavazi, malazi,kushiriki, kupata jina zuri, chakula na ulinzi.
Katiba iweke msisistizo na kutamka kuwa watoto wenye ulemavu wa ngozi
wanastahili kupata ulinzi maalumu, kuwa na shule maalumu ambazo ni za bweni na
wanapokwenda kwenye mikusanyiko kama mikutano mikubwa wapewe ulinzi na vyombo vya
usalama na pia anapokuwa mmoja mmoja apewe msaidizi. Pia katiba itoe tamko kuwa
hawa watoto wenye ulemavu wapewa huduma kama vifaa vya kusomea na mafuta kwa
ajili ngozi.
Watoto wenye ulemavu wa viungo wana haki ya kupata viungo bandia,
baiskeli, elimu, huduma za afya na kuhakisha majengo yanayotoa huduma muhimu ni
rafiki kwa walemavu.
Pia katiba itamke kuwa watoto
wenye ulemavu wa macho, wanahitaji vifaa vya kusomea, maandishi ya nukta nundu,
fimbo za kutembelea, walimu wa kutosha wenye utaalamu wa kuwafundisha watoto hao.
Pia katiba izungumzie kuwa watoto wenye ulemavu wa kutosikia
wanahitaji walimu wenye ujuzi katika mafunzo
ya lugha za ishara.
4.MABARAZA YA WATOTO YA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA KUTAMBULIKA KIKATIBA.
Tunapendekeza
katiba mpya iweke kipengele cha kutambua mabaraza ya watoto na kutoa maelekezo
kwa serikali kuanzisha mabaraza kuanzia ngazi ya mtaa/ kijiji hadi taifa na
kutenga rasilimali za kuendesha mabaraza hayo. Hii itawapa nafasi watoto kukusanyika mahali
pamoja, kushiriki na kutoa maoni juu ya masuala yanayowahusu ambayo ni haki yao
kikatiba.
5. WATOTO KUWA NA MBUNGE WAO WA KUWAWAKILISHA BUNGENI
Kwa
kuwa watoto ni zaidi ya nusu ya idadi ya watanzania wote na wana mahitaji mengi
yanayohitaji kupewa kipaumbele na taifa. Katiba mpya iweke mfumo wa wawakilishi
wa watoto bungeni kwa kutoa nafasi 2 za wabunge mmoja kutoka Zanzibar na mmoja
kutoka Tanzania Bara wa kuzungumzia masuala yanayowahusu watoto. Katiba itoe
tamko kuwa wabunge hao (2) wateuliwe na Raisi kwa kuwashirikisha watoto wa Baraza
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
6. VYETI VYA KUZALIWA KWA
WATOTO.
Kumekuwepo
na tatizo kubwa la upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa , na tatizo hili linatokana na baadhi
ya wazazi kushindwa kupata fedha za kulipia gharama zilizowekwa kupata cheti
cha kuzaliwa, pia sababu nyingine ni kwamba hizo huduma ziko mbali sana na
wananchi hali ambayo inapelekea usumbufu
kwa wazazi kutembea umbali mrefu au kuingia gharama kufuata vyeti hivyo kwenye
ofisi ya mkuu wa wilaya.
Hivyo
basi tunaomba katiba itamke watoto wote kuanzia umri wa miaka 0-17 badala ya
miaka 0 - 5 wapatiwe vyeti bure bila mzazi kulipia gharama yeyote.
Pia
tunaomba katiba itamke na kutoa mamlaka kwa vituo vya afya, zahanati na
hospitali kutoa vyeti vya kuzaliwa.
7. MFUMO WA ELIMU.
Mfumo
wa elimu uliopo sasa unaleta ubaguzi kati ya watoto wanaotoka kwenye familia
zenye kipato kizuri na familia duni au maskini. Mfano watoto wanaosoma shule za
binafsi au ‘English medium school’ wanafanya vizuri zaidi katika masomo hasa
sekondari na wengi wao wanaotoka kwenye familia zenze kipato bora na wale
wanaotoka familia duni au maskini wanasoma kwenye shule za kawaida ambapo elimu
sio bora. Lugha inayotumika kufundishia ni tofauti, uwezo wa walimu ni tofauti
na gharama zinazolipwa kwenye hizo shule ni kubwa ambapo mzazi wa kawaida
hawezi kulipia
Kutokana
na hali hii tunaomba Katiba itamke kuwa lugha ya kufundishia iwe ya kiingereza
katika shule zote kuanzia awali, mitaala yote ya kufundishia iwe sawa na muda
wa kubadilishia mtaala uwe mrefu angalau miaka 10 ili tuone matunda ya mitaala
hiyo. katiba itoe tamko kuwepo mfumo
maalumu wa kitaifa wa kubadilisha
mitaala na mfumo huo uwashirikishe wadau wa elimu wakati wa kufanya
marekebisho kwenye mitaala. Pia katiba itamke uwepo wa taasisi au bodi
maalumu ya kuratibu gharama za uendeshaji wa shule za sekondari, misingi na elimu
ya juu (vyuo vikuu)
8.MFUMO WA HUDUMA ZA AFYA
Katiba
mpya itamke wazi huduma za afya kwa watoto zitolewe bure kuanzia miaka 0 -17,
na itoe maelekezo kwa serikali na sekta husika kuweka mifumo ambayo itasaidia
huduma hizo kupatikana bure. Mfano
uchangiaji wa bima za afya ngazi ya kaya. Ili kuboresha afya ya mama na
mtoto tunaomba katiba itamke kuwa mama anapojifungua apewe likizo ya miezi 6
ili aweze kumunyonyesha mtoto miezi 6 mfululizo bila kumpa chakula chochote
tofauti na ilivyokuwa awali, hii itasaidia wanawake kupata muda mzuri wa
kuwa karibu na kuwanyonyesha watoto wao kwa muda wa kutosha.
9.MASUALA YA MUUNGANO
Suala
la elimu ya awali hadi sekondari liwe la muungano, kusiwepo utofauti wa mitaala
kati ya Tanzania visiwani na Tanzania bara ili kuweka usawa katika ufahamu na
uelewa wa watoto na taifa kwa ujumla.
10.SHERIA , SERA , MILA NA
DESTURI ZINAZOVUNJA HAKI ZA WATOTO
Katiba
mpya itamke wazi sheria, sera na taasisi zote zinazokiuka na kuvunja haki za
watoto zifutwe. Kwa mfano sheria au sera ya elimu inayotamka kumfukuza mtoto wa
kike anapopewa mimba wakati akiwa shuleni, imegundulika kwamba watoto
wanaoachishwa shule au kufukuzwa shule kwa ajili ya mimba wanaishia mitaani,
wengine wanaamua kuolewa wakiwa na umri mdogo mwisho wa siku tutakuwa na taifa
lenye watoto wa kike wengi wasiokuwa na mwelekeo wa kimaisha au wasiokuwa na
elimu. Kupata mimba kisiwe kigezo cha kumvunjia mtoto haki yake ya kusoma.
Kutokana na hili suala tunapendekeza katiba iweke kipengele cha kufuta sheria ya Elimu inayotamka kuwa mtoto wa kike
akipata mimba afukuzwe shule na kurudisha nyumbani pia itoe tamko moja kwa moja
kuwa mtoto akipewa mimba arudi shule, katiba itoe maelekezo ya kumrudisha mtoto
shule nyingine ili aweze kuendelea na masomo.
Sheria
ya Ndoa ya mwaka 1971 inapelekea watoto kuvunja haki zao kwa kuwa inamruhusu
mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi na wakiume
kuoa akiwa na umri wa miaka 18, kwa kuwa vitendo vya watoto wa kike kuolewa
wakiwa wadogo vimekidhiri, taifa halihitaji tena kuwa na sheria hiyo kwani
inakinzana na sheria nyingine kama vile sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ambayo imeanisha umri wa mtoto na majukumu ya
mtoto, pia inatoa ubaguzi na kuonekana inamkandamiza na kumbagua mtoto wa kike
kwanini imruhusu mtoto wa kike kuolewa na umri wa miaka 15 na mtoto wa kiume
kuoa akiwa na miaka 18. Pia kuendelea kuwepo kwa sheria hiyo kutawapa fursa
wazazi kuendelea kuwaozesha mabinti zao badala ya kuwaendeleza kwa vile sheria
inawalinda. Hivyo Basi tunapendekeza katiba ije na tamko la kuwa umri wa
kuolewa au kuoa ni miaka 18 na itoe tamko la kufutwa sheria ya ndoa kama
itakuwa haijabadili kipengele hicho ndani ya mwaka mmoja tangu kutungwa kwa
katiba.
Sheria
ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka1998, watoto tunatambua kuwa kuna marekebisho
madogo yaliyofanywa kwenye sheria hiyo baada ya kutungwa kwa sheria ya mtoto
mwaka 2009 hasa kwenye adhabu kwa mtoto aliyefanya kosa la kujamiiana mtoto mwenzake.
Ila kipengele kinachotamka kuwa mtu hatahesabika amembaka msichana mwenye umri
wa miaka 15 ikiwa amejamiiana naye wakiwa katika ndoa ambayo wazazi wameridhia
hakikufanyiwa marekebisho kipengele hiki kinaendelea kulinda kile kipengele
kilicho kwenye sheria ya ndoa kinachomruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka
15 kuolewa. Tunaomba katiba itamke kufutiliwa mbali kipengele hicho kwani
kinaendelea kunyima haki mtoto kwa kumshirikisha kwenye vitendo vya ngono akiwa
mdogo.
Sheria
na miongozo ya Elimu iliyopo kwa ajili ya matumizi ya adhabu ya viboko
mashuleni. Suala adhabu ya viboko mashuleni zimekithiri na walimu wanatoa
adhabu ya viboko bila miongozo iliyopo hadi kufikia watoto kuchapwa bila kufahamu
kosa lake. Adhabu nyingine mbaya kwa watoto ni pamoja na watoto kuchimba
mashimo, kung’oa visiki, kupiga magoti na kufyatua tofali. Adhabu hizo zinamuathri mtoto kimwili na
kisaikolojia pia kumdhalilisha mtoto ambavyo ni kinyume na
haki za mtoto zilizoainishwa kwenye sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa zinazozuia
kumjeruhi mtoto kimwili, kumdhalilisha na kufanyiwa vitendo vya ukatili vyenye
kumshusha utu na hadhi kwa mtoto. Hivyo tunaomba katiba itoe tamko la kufuta
hiyo miongozo na sera hizo kwani zinatoa mwanya mkubwa kwa walimu kuendelea
kuwanyanyasa watoto. Pia katiba itoe tamko kwa jamii kuacha mila au utamaduni
zinazoleta madhara kwa mtoto, kwa mfano suala la viboko na adhabu kali
zimeonekana pia zikitolewa na wanafamilia, na ni utaratibu umekuwepo kizazi
hadi kizazi.
11. TUME YA TAIFA YA HAKI ZA WATOTO
Katiba
mpya iunde tume huru ya kudumu ya taifa ya haki za mtoto yenye utaalamu wa
kushughulikia haki za watoto ikiwa ni pamoja na kusimamia, kupokea
taarifa, kufuatilia uvunjwaji na kutoa
mapendekezo juu ya hatua za kuchuliwa na serikali au taasisi dhidi ya ukiukwaji
wa haki za mtoto. Pia itoe maelekezo ya uundwaji wa kamati mbali mbali
zinazoshughulikia masuala ya watoto kuanzia ngazi ya mtaa/ kijiji hadi mkoa
zitakazo fanya kazi kwa karibu na tume.
12.ULINZI
WA WATOTO AMBAO HAWANA MAKAZI MAALUMU,NA WALE WAISHIO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI.
Katiba
itoe tamko kuhusu utekelezwaji wa mifumo
ya ulinzi wa mtoto iliyoko nchini mfano ule mpango mkakati wa ulinzi wa mtoto
kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa ya kushughulikia masuala ya watoto waishio katika mazingira hatarishi au
maelekezo kwa serikali na sekta husika
kuweka mfumo maalumu juu ya ulinzi wa watoto ambao hawana makazi maalumu na
waishio katika mazingira hatarishi.
13.KUWEPO NA WIZARA
YA WATOTO TU.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inayoshughulikia masuala
ya watoto hivi sasa imeelemewa na mambo mengi na hata bajeti inayotengewa kwa
ajili ya wizara hiyo haikidhi mahitaji ya watoto. Hivyo tunapendekeza katiba
mpya ije na tamko la kuunda wizara maalumu kwa ajili ya watoto kwani vile watoto
ni sehemu kubwa sana ya watanzania wote kwani zaidi ya nusu ya watanzania ni
watoto kwanini tuchanganywe na na wizara zingine?
HITIMISHO
No comments:
Post a Comment